Saturday, August 24, 2013

Viwanda vya mikate vyafungiwa

SHIRIKA la Viwango nchini (TBS), imefungia viwanda vitatu vya kutengeneza mikate katika Manispaa ya Dodoma kutokana na kufanya kazi bila kuthibitishwa huku mazingira yakiwa machafu. Zoezi hilo liliendeshwa jana na Maafisa wa TBS ambazo viwanda vya kuzalisha mikate vilivyofungiwa ni Capital, Kizota na Mnasi. Katika kiwanda cha Capital hali ya mazingira ilikuwa si ya kuridhisha huku mikate ikitengenezwa karibu na choo ambacho kilikuwa hakina bomba wala sehemu ya kunawia mikono huku wafanyakazi wakiwa wamevaa ndala na sare chafu. Mmoja wa wasimamizi wa kiwanda hicho, Rashid Ally alisema walikuwa wakifanya utaratibu wa kuhamia kwenye jengo la kisasa lakini kwa bahati mbaya TBS wamefika na kuwakuta wakiendelea na uzalishaji kwenye jengo hilo ambalo wamepanga. Alisema walianza kuzalisha mikate mwaka 2008 na walikuwa wakifanya biashara bila kuthibitishwa na TBS kutokana na kutojua utaratibu. Kwa upande wake, Meneja na Kiwanda cha kuzalisha mikate cha Kizota ,Hamisi Fundi alisema zoezi hilo litafanya wasimamishe uzalishaji. “Ni kweli tulikuwa hatujafikia matakwa ya kisheria ili kufanya uzalishaji wa mikate lakini sasa tumejifunza nini cha kufanya” alisema Akizungumza mara baada ya zoezi hilo Afisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile alisema Aprili mwaka huu walitoa tangazo na kutaka wazalishaji wa mikate wahalalishe bidhaa wanazozalisha. Hata hivyo alisema muitikio ulikuwa mdogo na sasa wameanza kufanya ukaguzi mikoa mbalimbali nchini. Alisema katika nchi nzima kuna viwanda 15 tu vya kutengeneza mikate vilivyosajiliwa na TBS huku wazalishaji wengi wa mikate wakifanya kazi kiholela bila kufuata utaalam na kujali usafi wa mazingira ya uzalishaji. Alisema Dar es Salaam ina viwanda sita vilivyosajiliwa, Arusha vitatu, Tanga viwili, Kagera viwili, Moshi kimoja na Morogoro kimoja. Aliitaja mikoa ambayo tayari wamefanya ukaguzi kuwa ni Tanga, Arusha, Dar es Salaam na Dodoma na kilichoonekana ni viwanda vingi havijathibitisha ubora wa viwango vinavyotakiwa katika kuzalisha mikate. “Ubora wa mikate ni pamoja na usafi wa mazingira, mikate imekuwa ikizalishwa katika mazingira yasiyo safi na salama na hivyo kutishia usalama wa afya za walaji” alisema Alisema mikate mingi inayotengenezwa na kuuzwa haioneshi muda wa matumizi utakwisha lini, imetengenezwa kwa kutumia nini na haina hata sehemu inayoonesha ina uzito gani. Alisema viwanda hivyo vitafunguliwa mara baada ya kukamilisha taratibu zote na kukidhi matakwa ya TBS Kwa upande wake, Mwanasheria wa TBS, Baptister Bitaho alisema sheria ya viwango namba 2 ya mwaka 2009 inakataza kupeleka bidhaa zenye viwango hafifu sokoni. Alisema operesheni hiyo itakuwa endelevu na kuwataka wazalishajio wote wa mikate kufuata sheria.

No comments:

Post a Comment