MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu (Chadema) ambaye anatuhumiwa
kumjeruhi Askari wa bunge jana hakufikishwa mahakamani kama ilivyotarajiwa huku
Jeshi la polisi likisema linaendelea na upelelezi.
Mbunge huyo jana aliripoti Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Dodoma kutokana
na tuhuma zinazomkabili za kumjeruhi Askari wa Bunge.
Mbilinyi anadaiwa alimpiga kichwa pamoja na ngumi na kumjeruhi
jicho la upande wa kulia Koplo Nikwisa Nkisu.
Aliripoti makao makuu ya polisi
kama alivyopangiw huku akiwa ameambatana na wakili wake ambaye ni Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Akizungumza mara baada ya kuripoti kituoni hapo, Lissu alisema polisi wanaendelea
na upelelezi na watawasiliana nao baada ya wiki mbili.
Kwa mujibu wa Lisu Jeshi la polisi limesema linaendelea na upelelezi na
watatoa taarifa lini watakuwa tayari ikiwemo maamuzi watakayochukua kama
kuendelea na kesi au la.
Hata hivyo alisema atashangaa kama polisi watafungua kesi kwa sababu kwa
mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 100 (2), inaeleza Mbunge hatashitakiwa au
kufunguliwa jinai lolote kwa jambo atakalofanya au kusema ndani ya Bunge, hii
inamaanisha katika viwanja vyote vya Bunge.
Alisema anamshangaa Naibu Spika Job Ndugai kwa kupigia kelele suala hilo liende wanaopiga
kelele hili jambo liende mahakamani.
Lisu alisema kisheria Sugu hawezi kushtakiwa na kwamba kinachofanyika ni
mashinikizo ya watawala.
Kwa upande wake Sugu alisema kinachofanyika sasa kinatokana na
alichokiita uhuni wa Ndugai.
Alisema kilichotokea bungeni kilikuwa ni maagizo ya Ndugai kwa kuwa
alisikika akisema huyo Sugu anajifanya mjanja mtoeni nje akome.
Alisema vitendo vyao
havijatukatisha tamaa, tutakomaa, hatuogopi sio tu kupigwa bali hata kuuwawa
kwa kutetea maslahi ya umma.
Sakata hilo la Sugu lilitokana na vurugu zilizotokea katika ukumbi wa
Bunge baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kupigana hadharani na askari wa
Bunge.
Wabunge hao walichapana ndani na nje ya ukumbi, hali iliyosababisha
tafrani kubwa, huku maofisa usalama na askari polisi kutoka kituo kikuu mjini
Dodoma, wakilazimika kuitwa kwenda kuongeza nguvu ili kukabiliana na hali hiyo.
Vurugu hizoo zilizuka baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe kunyanyuka ili kutaka kutoa hoja, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
alimtaka kukaa chini hali iliyowafanya wabunge wote wa upinzani kunyanyuka
wakiashiria kumuunga mkono.
Katika vurugu hizo ‘Sugu’ inadaiwa alimpiga kichwa pamoja na ngumi na
kumjeruhi jicho la upande wa kulia Koplo Nikwisa Nkisu.
Aidha chanzo cha vurugu hizo ni madai ya wabunge kutoka vyama vya
Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi kutaka
kuahirishwa kwa muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwa mchakato wa
kuandaliwa kwake haukuwashirikisha Wazanzibar.
No comments:
Post a Comment