Thursday, January 30, 2014

John Malecela amtaka mbunge Lowassa kuacha kukiuka misingi ya Chama



malecela akizungumza leo nyumbani kwake

WAZIRI Mkuu Mstaafu na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), John Samwel Malecela amemtaka Mbunge wa Monduli Edward Lowasa kuacha kuanza mbio za urais kabla ya wakati kwani anakiuka misingi ya katiba ya Chama.

Alisema hayo leo wakati wa Mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika nyumbani kwake Kilimani Mjini Dodoma ambapo pia alionesha fulana ambazo zimekuwa zikisambazwa nchi nzima zilizoandiwa 'Friends of Edward Lowassa.

"Chama sasa kinataka kutekwa na wenye fedha kwa uchu wa madaraka, mpaka tunashangaa na kujiuliza fedha wanatoa wapi? Na hayo madaraka wanayotaka kwa kununua ni kwa maslahi ya nani huku Watanzania
wakiendelea kuwa maskini" alisema Malecela wakati wa mkutano huo.

Malecela ameitaka Sectretatieti ya CCM kumjadili Lowasa kutokana na vitendo hivyo kwa sasa ni kukiuka misingi ya katiba ya chama.

Alisema  anamuuanga msemaji wa UVCCM),Paul Makonda kwa kitendo chake cha kumkemea Lowasa bila uoga kwa jinsi anavyokivuruga chama kwa lengo la kutaka Urais 2015 huku sekretarieti ikiwa kimya.

"Hapa najiuliza kuwa ile misingi imara ya uongozi ndani ya chama chetu cha mapinduzi iko wapi, mpaka tumuachie mtoto ndiyo akemee hayo hapa chama kipo wapi?" alihoji Malecela

Alisema vijana wanachama wamekuwa njia panda huku wakitamani kusikia tamko au karipio la chama juu ya suala hili la harakati za urais bila mafanikio.

"Kinachonisikitisha zaidi ni kuona juhudi za viongozi wa sasa wa chama ngazi za juu ikiwa ni pamoja na sekretarieti inayoongozwa na katibu mkuu Abdulahaman Kinana na Katibu Mweneze Nape Nnauye za kutetea chama zinatiwa mchanga" alisema.

 Alitaka juhudi zao zisibezwe na watu wenye nia njema na chama kwani wamekuwa na juhudi kubwa sana ya kujenga na kuimarisha chama kwa wananchi kila pembe ya taifa kwa kukemea na kuelezea misingi ya
uongozi bora.

"Sisi tulikijenga chama hiki kwa tabu sana na hapakuwa hata mtu mmoja aliyediriki kutumia fedha zake kutaka madaraka, nidhamu na busara na uchungu wa raslimali za taifa hili kwa maslahi ya wananchi ndiyo
vilivyotuongoza kufuata misingi na maadili ya uongozi ndani ya chama na Serikali.

 "Wakati wa kuanza mbio hizi bado na kufanya hivi kwa sasa ni kukiuka misingi ya katiba  amekamekemea tabia  ya baadhi ya watu ndani ya chama walioanza kuonyesha nia ya kuutaka urais kwa kutumia fedha zao
kinyume na misingi na katiba ya chama.

Mbali na hilo amesema kuwa wakati watu hao wakifanya hivyo, sekretarieti ya chama hicho imekaa kimya wakati inajua kuwa muda wa kuanza mbio za urais bado.

Akizungumzia suala la malumbano ndani ya chama, alisema kuwa vitendo hivyo havijana tija kwa chama.

Alisema hivi karibuni baadhi ya viongozi wa chama ngazi ya juuwamejibishana kwenye vyombo vya habari, vitendo hivi havina tija kwa chama na wala havileti umoja na mshikamano ambao umedumu ndani ya
chama kwa muda mrefu,"

"Ninaomba sekretarieti ichukue hatua haraka kama alivyoomba kijana wetu Makonda na kweli kuchelewa kuchukua hatua jambo hili kumejionyesha wazi kwamba utaleta kutoelewana ndani ya chama kusiko
kuwa na lazima,"alisema Malecela.

 

Akijibu maswali kwa waandishi baada ya kuuliza kukemea Lowasa peke yake wakati kuna wengine wanaofanya hivyo, Malecela alisema kuwa yeye hawajui hao wengine anamjua Lowasa na kuingia ndani na kutoa fulana mbili moja ikiwa na rangi nyeusi na kahawia na nyingine yenye rangi
nyekundu na nyeupe zikiwa zimeandikwa 'Friends of Edward Lowasa'.

Malecela alisisitiza kuitishwa kwa  kikao cha sekretarieti ili kutafakari jambo hilo ili litafutiwe dawa.

Hata hivyo alisema hawezi kulizungumzia suala la mawaziri mizigo kwani ni mambo yaliayoanzia bungeni nab ado yanaendelea kuzungumzwa. Alisema hata enzi za TANU watu walikuwa wakiokota maneno ya kusambaza na lile.

Alipoulizwa kwa nini akiwa kama mjumbe wa baraza la ushauri la CCM amekabiliana vipi na suala hilo, Malecela alijibu kuwa ameongea kama John Samwel Malecela ambaye amekuwa makamu mwenyekiti wa CCM kwa miaka 15 na anaongea kama mwanachama mwenye uchungu na nchi yake.."Baraza limeundwa chini ya Ibara ya 127 ya katiba ukisoma utaona nini kazi ya baraza, ina nguvu gani na inaelekeza kufanya nini" Alihoji
Malecela

Wednesday, January 29, 2014

Watanzania wahimizwa kutumia UDOM kujifunza masuala ya China

MKUU wa mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi  amekitaka Chuo Kikuu cha Dodoma
kutumia taasisi yake ya Confucius  (CIUDOM) kufunza watanzania utamaduni na
tabia za china kwa lengo la kuwawezesha watanzania kutumiakikamilifu  fursa
za kiuchumi zilizopo China kwa kujiamini na kujinafasi.

Dk Nchimbi alitoa kauli hiyo juzi wakati wa tamasha linaloambatana na
sherehe za mwaka mpya wa Kichina kwa mujibu wa kalenda ya taifa hilo.

Mwaka mpya wa Kichina mwaka huu umeadhimishwa Januari 27 kwa mujibu wa
kalenda iliyozoeleka.

Pamoja na kupongeza chuo hicho kwa kuandaa sherehe hiyo, mkuu huyo wa mkoa
alisema kwamba amefurahishwa sana na kuwapo na sherehe hizo ambazo
zinakumbusha pia mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na China.

Dk  Rehema ambaye alielezea kuridhishwa kwake na UDOM kupitia taasisi yake
ya CIUDOM kwa kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo hicho
katika kuwatamadunisha watanzania, aliwataka watanzania kutumia nafasi
zilizopo UDOM kujifunza lugha ya kichina na utamaduni wake ili kukabiliana
na fursa za kiuchumi za taifa hilo kubwa duniani.

Alisema kwa kujua lugha ya kichina na utamaduni wake watanzania watakuwa na
nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika uchumi wa China na kujipatia
manufaa makubwa.

Alisema wananchi wa Tanzania  wanastahili kutumia uwapo wa taasisi
inayofunza masuala ya China ili kujiongezea maarifa kutokana na ukweli kuwa
uchumi wa China unazidi kukua na Tanzania ina nafasi katika ushiriki wake.

Naye makamu mkuu wa chuo Profesa Idris Kikula alisema katika hotuba yake ya
kumkaribisha mkuu wa mkoa kwamba, Chuo hicho kimeingia matapatano ya
kuanzishwa kwa taasisi ya Confucius ikitambua kuwa ni nyenzo muhimu kufikia
ustawi wa watanzania.

Alisema katika kutambua uchumi wa China , urafiki uliopo na hali ya baadae
ya wafanyabiashara wa Kitanzania kwa kuzingatia shughuli nyingi za kiuchumi
zinazofanywa na China kusaidia maendeleo nchini China, UDOM pamoja na
kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzisha wa CIUDOM pia iliandaa  tamasha
hilola majira ya michepuo China kuenga kuungana na wachina katika
kusherehekea mwaka mpya na pia kujifunza mambo kutoka kwa raia wa China
waliopo nchini.

Katika mahojiano baadaye kuelezea maana yake, Profesa Kikula alisema kwamba
ifikapo mwaka 2030 China itakuwa nchi yenye uchumi mkubwa pengine kuliko
taifa lolote lile duniani, na kutokana na uchumi wake kuwa mkubwa, mengi ya
mataifa yatakuwa yanafanyabiashara na China na watanzania hawastahili
kukosa nafasi kutokana na ukaribu uliopo kati ya mataifa hayo mawili tangu
enzi za awamu ya kwanza ya uongozi baada ya Uhuru wa Tanzania.

Ni dhahiri katika hili kuwepo kwa taasisi inayofundisha nadharia za
Confucius kutasaidia kuiandaa Tanzania kufanya biashara kisahihi na China.

Kwa maneno yake mwenyewe profesa Kikula anasemaa kuanzishwa kwa taasisi
hiyo ni maandalizi ya kuwafanya watanzania washiriki kikamilifu katika
uchumi wa dunia ambao kufikia mwaka 2030 ni dhahiri utatawaliwa na China.

Alisema kuufahamu utamaduni wa China na lugha yao kutasaidia hata kuondoa
uwezekano wa kutapeliwa na wajanja wachache ambao wanatumia watanzania
kutoelewa lugha ya Kichina katika masuala ya biashara.

Katika kujifunza utamaduni wa Kichina kupitia nadharia za Confucius
watanzania wanapata nafasi  ya kujifunza utamaduni wa kichina uliowawezesha
kuwa na uchumi mkubwa katika kipindi cha muda mfupi. Aidha watajifunza
busara mbalimbali ambazo zikitumiwa zinaweza kutengeneza mfumo wa maisha
ambao pia utawanyanyua watanzania kifikira na kuwafanya wajitume maradufu.

Wachina wanaamini kwa mujibu wa mafundisho ya Confucius mtu akishindwa
lengo, dawa si kubadili lengo, bali kubadili njia au vitu vinavyosababisha
kushindwa ili kulifikia lengo husika.

Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dodoma (CIUDOM) kilizinduliwa rasmi
Aprili  28,mwaka jana na makamu wa rais Dk Mohammed Ghalib Bilal.Kuanzishwa
kwa CIUDOM kumeifanya tanzanuia kuwa moja ya nchi zenye taasisi zipatazo
400 za Confucius zilizotapakaa duniani kote.

Katika tamasha hili kikundi cha sanaa cha China cha Henan Art Troupe
kilifika na kuwatumbuiza wageni na wananchi wlaiohudhuria tamasha hilo.

mwisho

Saturday, January 18, 2014

Waziri Mkuu atembelea wahanga wa mafuriko

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda juzi alitembelea vijiji vya Chipogoro na Fufu katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino, mkoani Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali ambayo yaliathiriwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kati ya Januari 2 hadi Januari 11, mwaka huu.

Akiwa katika kijiji cha Chipogoro tarafa ya Rubi, Waziri Mkuu alikagua kituo cha polisi na nyumba zilizobomolewa, choo cha zahanati na kukagua eneo la barabara inayojengwa ya kutoka Dodoma hadi Iringa katika eneo lenye matatizo ya makaravati kuziba.

Kwenye kijiji cha Fufu katika tarafa ya Makangwa ambacho kiko umbali wa kilometa 30 kutoka Chipogoro, Waziri Mkuu alikagua maeneo ya makazi yaliyoathiriwa kwa mafuriko na kukagua baadhi ya nyumba zilizobomoka kabla ya kuzungumza na wananchi na kuwapa pole.

Akizungumza na wakazi wa vijiji hivyo mara baada ya kupokea taarifa za maafa ya mafuriko hayo, Waziri Mkuu alimtaka Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Eng. Leonard Chimagu kuhakikisha anasimamia wakandarasi wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake bado haujakamilika na kuainisha maeneo korofi ili yafanyiwe marekebisho haraka.

“Nimekagua matundu katika daraja moja pale Chipogoro na kuona ni madogo, mtaalamu anasema uchafu ulioziba ndiyo umesababisha maji yasipite. Mimi si mhandisi na hizi ni mvua za kwanza tu, sasa yakija maji mengi zaidi ya haya hali itakuwaje?, alihoji Waziri Mkuu.

“Hata hapa Fufu, kuna mahali nimeona maji yanaonyesha yalikuja kwa kasi kubwa lakini upenyo wa kuingia kwenye makaravati na kutokea upande wa pili ni mdogo sana... barabara hii ni mkombozi lakini kama haitazingatia uhalisia wa maeneo itakuwa ni balaa,” alionya.

Alimtaka pia awasimamie wakandarasi hao ili wanapoweka matoleo ya maji wahakikishe upande wa pili barabara maji hayo yanakwenda kwenye mikondo ya mto na siyo kuyaacha tu yasambae kiholela na kuishia kwenye makazi ya watu au mashamba yao.

Waziri Mkuu aliahidi kutoa mifuko ya saruji 2,600 na mabati 1,560 ambapo kila kijiji kitapata mifuko 1,300 na mabati 780 ili kuwasaidia wakazi waliobomolewa nyumba zao waweze kujenga nyumba za kisasa.

Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi kuwashirikisha wadau wengine katika mkoa huo ili waone wanawezaje kuchangia upatikanaji wa mabati mengi zaidi kwa ajili ya nyumba zilizoezuliwa.

Kuhusu chakula cha msaada, Waziri Mkuu alimtaka Dk. Nchimbi aandae makisio ya mahitaji ya chakula yaliyopo na kuyafikisha Ofisi ya Waziri Mkuu ambako kuna Idara inayosimamia maafa ili waletewe chakula hicho haraka kwa sababu kipo.

Alisema anakubaliana na ushauri uliotolewa kuhusu suala la ujenzi wa mabwawa ya kukinga maji ya mvua ili kupunguza kasi ya maji yanayoporomoka kutoka milimani lakini akasema Serikali imeanza na ujenzi wa Bwawa la Kidete lililoko wilayani Kilosa tangu yaliyopotokea mafuriko wilayani humo.

Awali akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Alfred Msovella, alisema nyumba 129 zilibomoka, vyoo 78 vimebomoka kikiwemo cha zahanati ambapo wakazi 1,390 wamepoteza vifaa mbalimbali ikiwemo vyakula, magodoro, vyombo vya ndani na mifugo.

Msovella ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa alisema hivi sasa, wakazi hao wanahitaji mahema 400, magodoro 381, madaftari ya wanafunzi na dawa za matibabu.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Fufu, alisema jumla ya nyumba 26 zilibomolewa na mali kama vyakula, samani, vyombo vya nyumbani na bidhaa za biashara kuharibika.

Alisema eneo la kijiji cha Fufu ni tambarare na liko chini ya safu za milima na maji ya mvua yanayoporoka kutoka milimani, huondoka polepole. “Hata hivyo, hali hii ya mafuriko imechochewa na ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami ambapo tuta la barabara mpya na vidaraja vidogo vilivyowekwa vimekuwa kizuizi cha maji mengi yanayotoka milimani na hivyo kuongeza tatizo la mafuriko,” alisema.

Mikutano hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu ambaye pia ni mbunge wa Mpwapwa pamoja na mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde
 

  • Waziri Mkuu Mizengo Pinda akijionea uharibifu uliofanyika kutokana na mafuriko yaliyotokea katika kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa Juzi.



Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiangalia athari za mafuriko katika kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa juzi


Wananchi mbalimbali wakiwa juu ya daraja katika eneo la Chipogoro



Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitoa maelekezo baada ya kutembelea eneo la Chipogoro juzi



Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiangalia athari za mafuriko yaliyotokea katika Kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa



Kondoo wakila mahindii yaliyoharibika kufuatia mafuriko yaliyokikumba Kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa



Mkazi wa Kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, Agness Mgongolwa ambaye ni miongoni mwa watu waliobomokewa na nyumba katika mafuriko yaliyotokea hivi karibuni


Thursday, January 9, 2014

Mkuu wa mkoa Dodoma apokea wasafiri wa treni

Abiria wa treni wakiandamana wakiwa nje ya Ofisi ya mkuu wa Dodoma
kusubiri kuwasilisha kero zao.

Waandishi wa habari wakawa kazini

Polisi wakituliza mzuka na kuhakikisha amani

Jamani taratibu

Saturday, January 4, 2014

Uozo stendi ya Daladala jamatini Dodoma

Mwajuma Salum maarufu Bibi Ndonga [64] akimlalamikia kwa kumuonyesha
Mhandisi msaidizi wa manispaa ya Dodoma Luanda stakbadhi ambazo
amekuwa akilipia katika kipindi cha miezi miwili bila kukabidhiwa eneo
la kuweka kibanda chake cha biashara na viongozi wa eneo hilo mhandisi
huyo alifika kuona utaratibu uliotumika kujenga vibanda vya biashara.


Mhandisi masaidizi manisaa ya Dodoma Luanda akitoa maelekezo kwa mama
lishe waliopo katika stendi ya Daladala ya Jamatini kujenga vibanda
sawa na vipimo vilivyowekwa sawasawa na utaratibu na sheria ndogo
ndogo za manispaa hiyo.


Askari wa kutuliza Ghasia wakiwa na mtutu wa Bunduki kusimamia
uhakiki wa vibanda vya wafanyabiashara katika stendi ya Daladala
Jamatini Dodoma kama utaratibu uliyowekwa ulifuatwa wakati wa ugawaji
na ujenzi.

Mmoja wa wafanyakazi katika ofisi ya Mhandisi wa manispaa ya Dodoma
akitoa amri ya kuondoa kimoja ya vibanda vilivyojengwa kiholela katika
stendi ya daladala jamati wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa vibanda vya
wafanyabishara.