WAZIRI MKUU Mizengo Pinda juzi alitembelea vijiji vya Chipogoro na Fufu
katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino, mkoani Dodoma na kukagua maeneo
mbalimbali ambayo yaliathiriwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zilizonyesha
kati ya Januari 2 hadi Januari 11, mwaka huu.
Akiwa katika kijiji cha Chipogoro tarafa ya Rubi, Waziri Mkuu alikagua
kituo cha polisi na nyumba zilizobomolewa, choo cha zahanati na kukagua eneo la
barabara inayojengwa ya kutoka Dodoma hadi Iringa katika eneo lenye matatizo ya
makaravati kuziba.
Kwenye kijiji cha Fufu katika tarafa ya Makangwa ambacho kiko umbali wa
kilometa 30 kutoka Chipogoro, Waziri Mkuu alikagua maeneo ya makazi
yaliyoathiriwa kwa mafuriko na kukagua baadhi ya nyumba zilizobomoka kabla ya
kuzungumza na wananchi na kuwapa pole.
Akizungumza na wakazi wa vijiji hivyo mara baada ya kupokea taarifa za
maafa ya mafuriko hayo, Waziri Mkuu alimtaka Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma,
Eng. Leonard Chimagu kuhakikisha anasimamia wakandarasi wa barabara hiyo ambayo
ujenzi wake bado haujakamilika na kuainisha maeneo korofi ili yafanyiwe
marekebisho haraka.
“Nimekagua matundu katika daraja moja pale Chipogoro na kuona ni madogo,
mtaalamu anasema uchafu ulioziba ndiyo umesababisha maji yasipite. Mimi si
mhandisi na hizi ni mvua za kwanza tu, sasa yakija maji mengi zaidi ya haya
hali itakuwaje?, alihoji Waziri Mkuu.
“Hata hapa Fufu, kuna mahali nimeona maji yanaonyesha yalikuja kwa kasi
kubwa lakini upenyo wa kuingia kwenye makaravati na kutokea upande wa pili ni
mdogo sana... barabara hii ni mkombozi lakini kama haitazingatia uhalisia wa
maeneo itakuwa ni balaa,” alionya.
Alimtaka pia awasimamie wakandarasi hao ili wanapoweka matoleo ya maji
wahakikishe upande wa pili barabara maji hayo yanakwenda kwenye mikondo ya mto
na siyo kuyaacha tu yasambae kiholela na kuishia kwenye makazi ya watu au
mashamba yao.
Waziri Mkuu aliahidi kutoa mifuko ya saruji 2,600 na mabati 1,560 ambapo
kila kijiji kitapata mifuko 1,300 na mabati 780 ili kuwasaidia wakazi
waliobomolewa nyumba zao waweze kujenga nyumba za kisasa.
Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi kuwashirikisha wadau
wengine katika mkoa huo ili waone wanawezaje kuchangia upatikanaji wa mabati
mengi zaidi kwa ajili ya nyumba zilizoezuliwa.
Kuhusu chakula cha msaada, Waziri Mkuu alimtaka Dk. Nchimbi aandae makisio
ya mahitaji ya chakula yaliyopo na kuyafikisha Ofisi ya Waziri Mkuu ambako kuna
Idara inayosimamia maafa ili waletewe chakula hicho haraka kwa sababu kipo.
Alisema anakubaliana na ushauri uliotolewa kuhusu suala la ujenzi wa
mabwawa ya kukinga maji ya mvua ili kupunguza kasi ya maji yanayoporomoka
kutoka milimani lakini akasema Serikali imeanza na ujenzi wa Bwawa la Kidete
lililoko wilayani Kilosa tangu yaliyopotokea mafuriko wilayani humo.
Awali akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Alfred
Msovella, alisema nyumba 129 zilibomoka, vyoo 78 vimebomoka kikiwemo cha
zahanati ambapo wakazi 1,390 wamepoteza vifaa mbalimbali ikiwemo vyakula,
magodoro, vyombo vya ndani na mifugo.
Msovella ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa alisema hivi sasa, wakazi
hao wanahitaji mahema 400, magodoro 381, madaftari ya wanafunzi na dawa za
matibabu.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Fufu,
alisema jumla ya nyumba 26 zilibomolewa na mali kama vyakula, samani, vyombo
vya nyumbani na bidhaa za biashara kuharibika.
Alisema eneo la kijiji cha Fufu ni tambarare na liko chini ya safu za
milima na maji ya mvua yanayoporoka kutoka milimani, huondoka polepole. “Hata
hivyo, hali hii ya mafuriko imechochewa na ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha
lami ambapo tuta la barabara mpya na vidaraja vidogo vilivyowekwa vimekuwa
kizuizi cha maji mengi yanayotoka milimani na hivyo kuongeza tatizo la
mafuriko,” alisema.
Mikutano hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory
Teu ambaye pia ni mbunge wa Mpwapwa pamoja na mbunge wa Mtera, Livingstone
Lusinde
![]() |
|
![]() |
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiangalia athari za mafuriko katika kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa juzi |
![]() | |
Wananchi mbalimbali wakiwa juu ya daraja katika eneo la Chipogoro |
![]() | |
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitoa maelekezo baada ya kutembelea eneo la Chipogoro juzi |
![]() | |
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiangalia athari za mafuriko yaliyotokea katika Kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa |
![]() | |
Kondoo wakila mahindii yaliyoharibika kufuatia mafuriko yaliyokikumba Kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa |
![]() | |
Mkazi wa Kijiji cha Chipogoro Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, Agness Mgongolwa ambaye ni miongoni mwa watu waliobomokewa na nyumba katika mafuriko yaliyotokea hivi karibuni |







No comments:
Post a Comment