Sunday, February 2, 2014

mamia waaga askari polisi waliokufa kwenye ajali


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi (SACP) David Misime jana aliongoza mamia ya waombolezaji
kuwaaga askari watano wa Jeshi la Polisi waliokufa ajalini  na kusema
vifo vya askari hao vimetokana na uzembe na mwendo kasi.
Alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuwasili kwa miili ya marehemu
hao ambayo iliharibika vibaya  kutokana na ajali hiyo hali
iliyopelekea  picha zao kuwekwa mbele za majeneza na watu kupita kutoa
heshima za mwisho.

Dodoma  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi (SACP) David Misime akizungumza jana

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma wakiwaaga askari watano waliokufa
ajalini
 
Waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni D.9084 Adolf Silla (51),F.6459
Evarist Bukombe (34),H.3783 Deogratius Mahinyila (29),WP.10337
Jackline Tesha (22) na WP.10382 Jema Luvinga.
Askari hao walikufa papo hapo usiku wa kuamkiajuzi baada ya gari
waliyokuwa wakisafiria T.770 ABT Toyota Corolla  kugongana uso kwa uso
na basi T.997 AVW Scania mali ya Kampuni ya Mohamed Trans.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mtumba nje kidogo ya Manispaa ya
Dodoma wakati askari hao wakitokea Dodoma kwenye sherehe za Polisi za
kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha 2014.
Kwa Mujibu wa kamanda Misime miili hiyo iliharibika vibaya  hali
iliyowalazimu madaktari wa hospitali ya Rufaa ya Dodoma kufanya kazi
ya ziada kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ili iweze kusafirishwa
hadi walikozaliwa askari hao.
Pia alitaka kila mtu kuwa balozi ili kuhakikisha ajali za barabarani
ambazo asilimia 75 zinasababishwa na uzembe zinakoma la sivyo
wataendelea kusingizia kuwa vifo hivyo vinasababishwa na Mwenyezi
Mungu.
 




Aidha aliwataka madereva kutumia utashi waliopewa kamaliza ajali hizo
kwa kutii na kuheshimu kanuni na sheria za usalama barabarani bila
hivyo ajali zitawamaliza nawataendelea kupoteza uhai kila siku.
Alisema  wakati mwingine watu wanakiharakisha kifo hasa pale unapokuwa
si mpango wa mungu kuondoka duniani kutokana na uzembe huo
" Hata ukiona gari lile lilivyoburuzwa unaamini kabisa
kilichosababisha ni mwendo kasi"Alisema Misime.
Alisema msiba huo ni mkubwa sana kwani umepoteza nguvu kazi,walinzi na
hivyo jamii kukosa watu wa kuwahudumia kutoka na idadi askari mmoja
kuhudumia idadi kubwa ya watu hivyo kwa kuondokewa na askari hao
watano ni pigo kubwa kwa jeshi la polisi.
Kamanda Misime alisema wakati umefika kwa jamii kubadilika wenyewe na
kuzingatia sheria za usalama badala ya kusubiri kusimamiwa na
kuongozwa na askari wa usalama barabarani kila wakati.
Kamanda Misime pia aliwaonya wanaobaki na kuangalia familia za
marehemu hao kuhakikisha hawanyanyasiki na wanapata haki zao zote na
kuwasaidia kwa hali na mali pale wanapohitaji msaada,  na si
kuwanyang'anya hata kile kidogo walichochuma marehemu ambao
wametangulia mbele ya haki.
Katika salamu za rambarambi kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini
(IGP), Ernest Mangu zilizosomwa kwa niaba yake na kamanda Misime
zilisema kuwa jeshi hilo limepoteza vijana wake ambao ni mashupavu na
tegemeo kubwa katika ulinzi na usalama wa nchi na mkoa wa Dodoma kwa
ujumla.
Kwa upande Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kongwa
Christopher Kangoye amesema  Mkoa wa Dodoma ni mkoa wenye amani ya
kutosha na imetokana na kazi nzuri inayofanywa na askari wakiwemo hao
waliotangulia mbele ya haki.
Alisema kifo cha vijana kama hao kinaondoa hazina ya nguvu kazi ya
katika nchi na kuongeza kuwa waombolezaji waliopo wanatosha kufikisha
salaam hizo kwa kukemea mauji ya kizembe ya aina hiyo.
Naye Mchungaji Japhet Sudayi wa kanisa kuu la toho mtakatifu Aglikani
Dodoma akihubiri katika ibada ya kuwaga marehemu hao amewaasa
waombolezaji kutofadhaika na kukufuru na badala yake wajitayarishe kwa
kutenda matendo mema yenye amani na furaha wakati wote.
Tayari miili hiyo imesafirishwa kwa ajili ya kwenda Mikoa ya Kigoma,
Kilimanjarom, Iringa, pamoja na Mpwapwa na Kongwa kwa ajili ya
mazishi.

No comments:

Post a Comment