Sunday, February 2, 2014

waomba TFDA iwapatie bidhaa feki kwani wanazihitaji



MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) kanda ya kati Dodoma juzi ileteketeza tani tatu za madawa, chakula na vipodozi ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu ambapo bidhaa zote zikiwa na thamani ya Sh. Milioni 19.
Katika hali ya kustaajabisha baadhi ya wakazi wanaoishi karibu na eneo la dampo la Mbwanga  ambao walikusanyika kushuhudia tukio  la kuteketezwa kwa bidhaa hizo walikuwa wakiomba wapatiwe bidhaa hizo ili waweze kuzitumia na hata kuziuza.
Baadhi ya wananchi hao ambao waliweka mikono kichwani kusikitika bidhaa hizo zikiteketezwa mbele yao walisema wako tayari kudhurika kuliko kuona pipi, blueband, maziwa ya kopo yakiteketezwa mbele yao ni heri wangepewa ili wakatumie..
Miongoni mwa bidhaa zilizoteketezwa ni masanduku 20 ya soda ambazo zilikamatwa kwenye moja ya maduka katika stendi kuu ya Dodoma ambazo zilikuwa kwenye friji.
Soda hizo zilikuwa zimeisha muda wake lakini walikuwa wakiuziwa wateja wa mabasi yanayosimama stendi ya Dodoma kitu ambacho wataalam wa TFDA wamesema ni hatari na kutaka abiria kuwa makini pindi wanaposafiri kwani kununua bidhaa kwa haraka wakiwa madirishani si salama kwa afya zao.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Kati, Florent Kyomo alisema zoezi hilo litakuwa endelevu kwa lengo la kuondoa bidhaa sokoni bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu.
Alisema mamlaka hiyo iwe macho  na wataendelea kukagua na hata baadhi ya wafanyabiashara waliowahi kukamatwa sasa wameamua kubadilika.
Kwa upande wake Mkaguzi wa dawa wa TFDA, Dk.Engelbert Bilashoboke alisema  kuna baadhi ya maduka ambayo yanauza dawa ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu hali inayopelekea mtumiaji kutumia dawa ambazo haziwezi kuponya magonjwa yake.
Alisema mnunuzi anaweza kuona amenunua dawa kumbe hata kile kilichoandikwa juu ya dawa si kile kilichomo ndani yake.
“Unaweza kuona ni dawa kumbe si dawa sahihi” alisema

Mkaguzi wa Chakula wa Mamlaka hiyo, Sifa Chamgenzi alisema madhara ya kula vyakula ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu ni makubwa.
“Unaponunua chakula unatumaini kitajenga na kuupa mwili nguvu lakini chakula kinapokuwa  kwa ajili ya kuleta madhara kwenye mwili hili linakuwa ni tatizo kubwa.
Alisema wanajitahidi kuelimisha watu waangalie vyakula vinavyofaa kabla ya kuvitumia kwa kuona muda wa kutengenezwa na muda wa mwisho wa matumizi yya vyakula hivyo ”alisema
Miongoni mwa bidhaa zilizoteketezwa ni pamoja na madawa ya binadamu, maziwa ya kopo, blue band, Tomato sauce, Soda, pipi, sabuni za kuoshea sehemu za siri za wanawake aina ya Kaisiki, sabuni za aina mbalimbali za kuondoa harara na upele, madawa ya Kichina kwa ajili ya kuchua na mafuta ya kupikia.

No comments:

Post a Comment