Friday, December 5, 2014

St John wajipanga kuondoa migogoro



KUFUATIA mgomo wa walimu na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha St John
cha Mjini hapa Mkuu mpya wa Chuo hicho Profesa Emmanuel Mbennah
amesema  wamejipanga  kuhakikisha changamoto zinazokikabili chuo hicho
 zinashughulikiwa  katika muda mfupi ujao.
Alisema hayo jana wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi
kufuatia mgomo wa walimu na wanafunzi unaoendelea chuoni hapo ambapo
walimu wamekuwa wakidai kuongezewa maslahi na wanafunzi wakitaka
kutengenezewa mazingira mazuri ya kusomea na kusajili wa kwa kozi
NACTE.
Profesa Mbennah alisema muda mfupi ujao chuo hicho kitakuwa mahali
bora na pazuri pa kutolea taaluma kwa wanafunzi na wahadhiri
mbalimbali kufanyia kazi, hivyo kuomba wapewe muda kuyashughulikia.
Alisema, uongozi uliopo ni sikivu na umepokea changamoto zote
zinazokikabili chuo hicho hususani kutoka kwa wanafunzi na wahadhiri
wote na upo tayari kuzichambua na kuzishughulikia mapema iwezekanavyo,
ili chuo hicho  kiwe mahali bora na pazuri pa kusoma na kwa wahadhiri
kufanyia kazi.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya kozi
kutokusajiliwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE), uchache wa
wahadhiri mbalimbali chuoni hapo na vitendea kazi vya kutosha
kufundishia ili chuo kiweze kutoa taaluma nzuri na bora.
Alisema, kulingana na mahitaji ya viwango vya kozi za kilimo na
maabara ya tiba za magonjwa ya binadamu katika kozi za ufundishaji
ngazi za cheti na astashahada, NACTE walitoa sharti la kukamilisha
chumba cha mafunzo kwa vitendo ili chuo kiweze kupata usajili wa kozi
hizo mbili.
Alisema tayari chumba hicho cha mafunzo kwa vitendo kimekamilika, na
jana alikikagua na kuridhika na mahitaji kama yalivyoainishwa na
NACTE, na tayari ameshauandikia  uongozi wa NACTE kuja chuo hapo ili
kukagua na kutoa usajili huo.
Pia katika kutatua upungufu wa wahadhiri chuoni hapo, chuo kinatarajia
kuajiri waaimu wapya Desemba mwaka huu na kwa sasa kinaendelea kutumia
baadhi ya wahadhiri kutoka vyuo vingine vya elimu ya juu vilivyopo
hapa Dodoma, kusaidiana na wahadhiri waliopo chuoni hapo.
Alisema walichokubaliana na uongozi wa serikali ya wanafunzi (SOSJUT)
kwa kushirikiana na uongozi wa Kaimu Mkuu wa Chuo Taaluma washirikiane
kutayarisha andiko maalumu litakalotumwa kwa baraza la chuolikielezea
mapungufu ya mfumo wa sasa yaliyopo na jinsi wanafunzi wanavyoathirika
na viwango hivyo vya zamani vya utoaji wa alama za ufaulu, kisha
yatajadiliwa na baraza la seneti na kuyatolea majibu.
Suala lingine la wanafunzi ni kuhusu kutosajiliwa kwa baadhi ya kozi
za fani ya kilimo na maabara za tiba. Mkuu huyo alisema kwamba, jambo
hili limeshakamilika  na NACTE muda wowote watafika kwa ukaguzi wa
maagizo waliyotoa kwa chuo ili yatekelezwe na kisha kutoa usajili.
Pia alitoa wito kwa wanafunzi wote katika fani hizi wasiwe na mashaka,
kwani muda mfupi ujao watakamilisha mafunzo yao na kupatiwa vyeti
vyao.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Daniel Damian alisema ni
muda mrefu palikuwa na mazungumzo kati ya uongozi wa chuo na serikali
ya wanafunzi kuhusu masuala mbalimbali na uongozi wa wanafunzi
uliwasilisha rasmi changamoto zao kwa uongozi wa chuo na kuahidiwa
kujibiwa.

No comments:

Post a Comment