Tuesday, March 31, 2015

Wanafunzi Vyuo Vikuu wakanusha kumshinikiza Lowasa Kugombea Urais

VIONGOZI wa Serikali za wanafunzi wa Vyuo Vikuu mkoani Dodoma wametoa
tamko la kulaani vikali kuhusishwa kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya
Dodoma kwa kumuomba Edward Lowasa agombee Urais katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akisoma tamko mbele ya Waandishi wa Habari,Rais wa  Serikali
ya Wanafunzi wa Chuo cha St John, Daniel Damian alikanusha Wanafunzi
wa Vyuo Vikuu vya Dodoma kwenda kwa Edward Lowasa kumshinuikiza
agombee Urais.
Alikuwa akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Serikali za Wanafunzi wa
Vyuo Vikuu vikiwemo Madini  (MRA)Chuo cha Elimu ya Biashara Tanzania
(CBE)Chuo cha Elimu ya Biashara (ASEK)Chuo cha Uuguzi Mirembe na
Kitivo cha Sayansi na Jamii cha UDOM.
Damian alisema wanapenda kukanusha vikali na kulaani  kuwa wao
wanatumiwa na Wanasiasa na wakiwa kama Wasomi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma
,hawatumiwi kwa jambo lolote na Viongozi wa Vyama vya Siasa.
 Alisema wao kama Viongozi wa Serikali za Wanafunzi kutoka vyuo Vikuu
vya Dodoma,wanapinga na kulaani kitendo cha watu wachache
wanatukiingiza katika Propaganda za Kisiasa.
Pia alisema wao kama wasomi ambao jamii inawategemea kama kioo
hawawezi kuandamana na kujikusanya kwenye nyumba ya kiongozi na
kumuomba ogombee urais wakati wanajua fika wao hawahusiki na uteuzi wa
wagombea ndani ya Taasisi yao.
Alisema kilichofanyika ni kuudanganya umma wa Watanzania kwa kupitia
kivuli cha Vijana wachache kutoka vyuo vya hapa Dodoma ambao walifanya
kwa sababu zao binafsi.
Alisema Mkoa wa Dodoma unavyuo visivyopungua nane na jumla ya
Wanafunzi wote wanaosoma katika Vyuo vya Dodoma ni zaidi ya wanafunzi
35,000 huku Chuo cha UDOM kikiwa na Wanafunzi wasiopungua 22,000 huku
idadi ya watu waliojikusanya ikiwa haizidi  230 wengi wakiwa ni
Wamachinga na Wenyeviti wa Jumuia ya Wazazi.
Pia alisema ukiwatoa Wamachinga na Jumuia ya Wazazi waliokuwepo idadi
wa Wanafunzi waliokuwepo katika tukio hilo ni sawa asilimia 0.4 ya
Wanafunzi wote wanaosoma Vyuo vya Dodoma.
‘’Tunasikitika na pia tunashangazwa na dhambi tusiyoitenda
tunayobebeshwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma ambao kwa sasa tupo
katika msimu mpya wa masomo wenye changamoto mbalimbali, ni jambo
lililotusikitisha sana ‘’
Alisema Taifa linatakiwa lifahamu hawapo tayari kutumia Elimu zao bali
wametoka Vijijini kuja kutafuta Elimu ili iwawezeshe kulikomboa Taifa
na sio kuwatumikia wanasiasa kwa malengo yao.
Waliwaasa Wanafunzi popote Nchini makundi maali mbali ya
kijamii,Wakulima,Wafugaji,Wavuvi.Wamachinga,Wasanii na Taasisi za Dini
kwamba watu wachache kuzungumza kwa niaba ya makundi yao.

Vijiji 20 Kondoa kunufaika na mradi wa ujenzi wa vyoo


VIJIJI 20  katika Wilayani kondoa mkoani Dodoma vinatekeleza mradi wa kuimarisha afya na usafi wamazingira ikiwa ni pamoja ujenzi wa vyoo bora ili kuwezesha wakazi wa maeneo husika kuondokana na na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa vyoo kwemye makazi yao.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wilayani Kondoa, John Tesha, wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya mradi wa Kuimarisha afya  unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uswiss kupitia mradi wa HPSS-Tuimarishe Afya.
Mradi huo wa Afya na Mazingira unatekelezwa na HPSS kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya kondoa katika vijiji 20.
Tesha alisema vijiji hivyo 20 viliwezeshwa kuandaa mpango wa kuboresha afya kwa njia shirikishi, pia jamii ilishiriki katika mchakato wa uchefushaji juu ya usafi wa mazingira ili kuweza kubadili tabia za jamii.
Pia kubainisha mahitaji ya vifaa mbalimbali kwaajili ya ujenzi wa vyoo bora.
Desemba mwaka jana mpango huo ulianza katika vijiji vitano ambapo wananchi hao walipewa vifaa kwa ajili ya ujenzi wa vyoo bora, kwakutumia mabampa (Latrine Slab) ambayo sasa yanatumika kujengea.
Katika vijiji hivyo kuna vikundi 20 ambavyo pia wanachama wake wamefundishwa namna ya kutengeneza mabampa na uendeshaji wa mfuko wa usafi ambapo vimefungua akaunti wanazotumia kutunza fedha zinazotokana na mabamba wanayouza katika kila kaya kwaajili ya ujenzi wa vyoo bora.
Mradi huo wa Tuimarishe afya HPSS umesaidia vifaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa vyoo bora kupitia mfuko wake wa masoko na mpango wa masoko ya usafi.
Wanavikundi hao wanauza mabampa haya kwa wananchi ambayo kubwa linaunzwa kwa sh.20,000 na dogo sh.10,000 na moja ya sifa ya choo bora ni kuwa na sakafu inayo safishika
 Katika hatua za awali vikundi vimetengeneza na kuuza jumla ya mabamba 403, ambayo tayari yamewezesha kuboresha vyoo ngazi ya kaya.
Pia kutokana na mradi huo kufanyika katika vijiji hivyo ambapo hakuna uwezekano wa kuwepo kwa sakafu inayosafishika wamebuni uwepo wa mabampa yanayoendana na mazingira yavijijini.
Alisema kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wananchi katika mradi huo ambapo zaidi ya kaya 300 zimeagiza  mafundi kuwatengezea mabamba.
Kutokana na kasi ya mradi huo kunauwezekano wa kuwezesha jamii nzima kufikia malengo ya kuhakikisha kaya zenye vyoo bora zinaongezeka kwa asilimia 50.
Takwimu za UNICEF/WHO (2012) zinaonyesha kuwa ni asilimia 16 tu ya Watanzania  walikuwa wanajisaidia sehemu nyingine tofauti na choo, na ni asilimia 34 wanatumia vyoo bora, lakini pia ni asilimia 47 ambao wanatumia vyoo visivyo kidhi sifa za choo bora. 

Monday, March 2, 2015

Walimuoza binti mdogo kusota rumande mpaka kesi iishe



MKE na Mume wanaotuhumiwa kumuoza binti wa miaka 10 jana walifikishwa
katika mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini huku mahakama ikifunga
dhamana yao hadi kesi hiyo itakapomalizika.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kumuozesha mtoto mwenye umri
wa miaka 10 ambaye ni binti yao.
Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Wilaya Dodoma Mjini , Mwajuma
Lukindo Mwendisha mashitaka wa Serikali Lina Magoma alidai washtakiwa
Stephano
Nyambuya (65) na mkewe Juliana Gidion (30) ambao ni wakazi wa kijiji cha Lionii
wilayani Bahi mkoani Dodoma walitenda kosa la kumuozesha mtoto aliye
chini ya miaka 15
Mwendesha mashitaka huyo alisema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo
kinyume cha  kifungu cha sheria namba 138  (2) cha kanuni ya adhabu
kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Magoma alisema wazazi na walezi hao waliamua kumuozesha mtoto aliye
chini ya umri huo kwa Joshua Mnamba mwenye umri wa miaka (25), ambapo
wote kwa pamoja walikana shitaka lao.
Hakimu  mkazi Lukindo alisema washitakiwa hao
wanatakiwa kuwa rumande kutokana na kusa walilotenda kutokuwa na dhamana
Alisema kifungu cha sheria namba 148 (5) a (i) kinachozuia dhamana kwa
watu wenye makosa kama hayo, hivyo washitawa watabaki
rumande mpaka kesi yao itakapokwisha.
Kesi hiyo itatajwa tena Machi 16, mwaka huu
Mnamba ambaye alimuoa binti huyo alifikishwa mahakamani hapo Februari
24, mwaka huu na yuko rumande.
Mshtakiwa huyo alishtakiwa kwa kosa la kubaka.
Kwa sasa motto huyo aliyeozwa amepata hifadhi kwa mkuu wa Wilaya ya
Dodoma Mjini Betty Mkwasa.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulifuatiwa taarifa zilizotolewa na
majirani kwa serikali ya kijiji na hatimaye Polisi na watuhumiwa
kufanikiwa kukamatwa.
Mtotohuyo alikuwa ameozwa kwa mahari ya Sh. 100,000 na mbuzi 12.

Mtoto wa miaka 10 aozwa, mume, wazazi washkiliwa na polisi



MTOTO  wa miaka 10 aliyeozwa kwa mahari ya mbuzi 12 na Sh. 100,000 ameokolewa kutoka mikononi mwa mumewe  Joshua Mnamba (25), baada ya majirani kutilia shaka vilio vya mtoto huyo nyakati za usiku licha ya mumewe awali kudai binti huyo alikuwa ni ndugu yake.
Tukio hilo la aina yake, limetokea katika Kijiji cha Ibihwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambapo binti huyo (jina linahifadhiwa) alisema aliingia kwenye ndoa hiyo baada ya kushinikizwa na mama yake na bibi yake.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Bahi Mkoani limekiri kupokea taarifa za tukio hilo ambapo mara ya kwanza liliripotiwa Februari 9, mwaka huu na kuanza upelelezi na hatimaye kuwatia mbaroni watuhumiwa wote.
Watuhumiwa hao leo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani watuhumiwa akiwemo baba wa mtoto huyoStephano Mkuta na mama yake Juliana Gidion (50) kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mtoto huyo amedumu kwenye ndoa kwa wiki mbili.
Majirani na nyumba alimokuwa akiishi mtuhumiwa wanasema mara baada ya kufika na binti huyo walikuwa wakihoji binti huyo ni nani lakini alikuwa akijibu kuwa ni ndugu yake cha kushangaza walikuwa wakiishi peke yao kama mume na mke.
Majirani hao ambao hawakutaka kutaja majina walisema walikuwa wakisikia kelele  usiku wa manane za mtoto ambaye alikuwa akilia jambo ambalo liliwashangaza.
“Usiku tulikuwa tukisikia kelele za mtoto akilia ikabidi tujihoji iwapo ni mtoto anayeishi na mtuhumiwa huenda alikuwa akimlazimisha kufanya nae mapenzi usiku”
Lakini baadaye majirani hao waligundua kuwa Mnamba alikuwa ameoa mtoto mdogo wa miaka 10 kwa mahari ya mbuzi 12 na fedha taslimu Sh. 100,000.
Jambo hilo lilionekana kuwakera wananchi ambapo mmoja wao, alitetajwa kwa jina la Dominick alienda Ofisi ya Kijiji akachukua mgambo akakamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Bahi ambapo alichukuliwa maelezo yake.
Mtoto huyo ambaye kwa sasa amepata hifadhi kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa anasema hajui kusoma wala kuandika kwani wazazi wake hawakumpeleka shule na alikuwa akikaa nyumbani kulea wadogo zake.
 “Sijapelekwa shuleni nina wadogo zangu sita mimi ndio mkubwa na wazazi wangu na bibi ndio walikuwa wakitaka niolewe lakini nilikuwa nikikataa mimi ni mdogo” alisema
Alisema alikuwa akiishi na wazazi wake eneo la Bahi sokoni na baada ya kuolewa alipelekwa Ibihwa kwa mumewe.
“Baba, mama na bibi walisema nenda ukaolewe, niliondoka lakini nguo niliziacha kwa mama nikakuta Mnamba anaishi peke yake tukawa tukawa tunaishi wote na tunalala pamoja” alisema
Alisema baadaye mumewe alikuja kukamatwa na polisi kwani alikuwa ameoa mtoto mdogo.
“Nilikuwa sipendi kuolewa lakini walinilazimisha” alisema.
Mtoto huyo alisema kwenye fedha za mahari ambazo zilitolewa na mtuhumiwa bibi yake alipata mgao wa Sh. 10,000
Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mkwasa ambaye kwa sasa ni mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambaye anamhifadhi mtoto huyo nyumbani kwake anasema tatizo la ndoa za utotoni katika wilaya hiyo ni kubwa lakini wananchi wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa kwa kutoa taarifa wanapoona kuna ndoa ya aina hiyo.
“Ninashukuru hamasisho langu limezaa matunda na wananchi wamehamasika na sasa wanatambua madhara ya ndoa za utotoni na wamekuwa mstari wa mbele kupinga” alisema
Alisema tatizo kubwa la ndoa hizo katika Wilaya ya Bahi linasababishwa na mila na desturi za kabla la wagogo ambapo wasichana huolewa wakiwa bado wadogo.
“Sasa hii ya kumuoa mtoto wa miaka 10 ni kiboko maana mtoto mwenyewe hata maziwa hana ana umbo dogo inasikitisha sana” alisema
Alisema tatizo hilo pia limekuwa likichangiwa na mwamko finyu wa elimu kwani wananchi wengi ni wafugaji wanajali zaidi mifugo kuliko binadamu na hata umaskini umekuwa ukichangia.
“Baba ana mtoto wa miaka 10 na anataka kupata fedha akaamua kumuoza binti yake ili apate mbuzi na fedha lakini haangalii madhara ambayo mtoto Yule anaweza kupata.” Alisema.
Hata hivyo mtuhumiwa, Mnamba alisema alilazimishwa ndoa hiyo na bibi wa mtoto aliyetajwa kwa jina la Ntolwa ambaye alisema mtoto huyo ni mkubwa na anaweza ndoa jambo ambalo lilifanya amchukue na kwenda kuishi nae.
“Mimi nilikaa na yule mtoto lakini alikuwa hatoshi, nikaenda nikamwambia bibi namrudisha mtoto kwani hatoshi, nikamrudisha kwa bibi yake lakini bibi akamrudisha tena kwangu” alisema mtuhumiwa