Monday, March 2, 2015

Mtoto wa miaka 10 aozwa, mume, wazazi washkiliwa na polisi



MTOTO  wa miaka 10 aliyeozwa kwa mahari ya mbuzi 12 na Sh. 100,000 ameokolewa kutoka mikononi mwa mumewe  Joshua Mnamba (25), baada ya majirani kutilia shaka vilio vya mtoto huyo nyakati za usiku licha ya mumewe awali kudai binti huyo alikuwa ni ndugu yake.
Tukio hilo la aina yake, limetokea katika Kijiji cha Ibihwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambapo binti huyo (jina linahifadhiwa) alisema aliingia kwenye ndoa hiyo baada ya kushinikizwa na mama yake na bibi yake.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Bahi Mkoani limekiri kupokea taarifa za tukio hilo ambapo mara ya kwanza liliripotiwa Februari 9, mwaka huu na kuanza upelelezi na hatimaye kuwatia mbaroni watuhumiwa wote.
Watuhumiwa hao leo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani watuhumiwa akiwemo baba wa mtoto huyoStephano Mkuta na mama yake Juliana Gidion (50) kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mtoto huyo amedumu kwenye ndoa kwa wiki mbili.
Majirani na nyumba alimokuwa akiishi mtuhumiwa wanasema mara baada ya kufika na binti huyo walikuwa wakihoji binti huyo ni nani lakini alikuwa akijibu kuwa ni ndugu yake cha kushangaza walikuwa wakiishi peke yao kama mume na mke.
Majirani hao ambao hawakutaka kutaja majina walisema walikuwa wakisikia kelele  usiku wa manane za mtoto ambaye alikuwa akilia jambo ambalo liliwashangaza.
“Usiku tulikuwa tukisikia kelele za mtoto akilia ikabidi tujihoji iwapo ni mtoto anayeishi na mtuhumiwa huenda alikuwa akimlazimisha kufanya nae mapenzi usiku”
Lakini baadaye majirani hao waligundua kuwa Mnamba alikuwa ameoa mtoto mdogo wa miaka 10 kwa mahari ya mbuzi 12 na fedha taslimu Sh. 100,000.
Jambo hilo lilionekana kuwakera wananchi ambapo mmoja wao, alitetajwa kwa jina la Dominick alienda Ofisi ya Kijiji akachukua mgambo akakamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Bahi ambapo alichukuliwa maelezo yake.
Mtoto huyo ambaye kwa sasa amepata hifadhi kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa anasema hajui kusoma wala kuandika kwani wazazi wake hawakumpeleka shule na alikuwa akikaa nyumbani kulea wadogo zake.
 “Sijapelekwa shuleni nina wadogo zangu sita mimi ndio mkubwa na wazazi wangu na bibi ndio walikuwa wakitaka niolewe lakini nilikuwa nikikataa mimi ni mdogo” alisema
Alisema alikuwa akiishi na wazazi wake eneo la Bahi sokoni na baada ya kuolewa alipelekwa Ibihwa kwa mumewe.
“Baba, mama na bibi walisema nenda ukaolewe, niliondoka lakini nguo niliziacha kwa mama nikakuta Mnamba anaishi peke yake tukawa tukawa tunaishi wote na tunalala pamoja” alisema
Alisema baadaye mumewe alikuja kukamatwa na polisi kwani alikuwa ameoa mtoto mdogo.
“Nilikuwa sipendi kuolewa lakini walinilazimisha” alisema.
Mtoto huyo alisema kwenye fedha za mahari ambazo zilitolewa na mtuhumiwa bibi yake alipata mgao wa Sh. 10,000
Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mkwasa ambaye kwa sasa ni mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambaye anamhifadhi mtoto huyo nyumbani kwake anasema tatizo la ndoa za utotoni katika wilaya hiyo ni kubwa lakini wananchi wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa kwa kutoa taarifa wanapoona kuna ndoa ya aina hiyo.
“Ninashukuru hamasisho langu limezaa matunda na wananchi wamehamasika na sasa wanatambua madhara ya ndoa za utotoni na wamekuwa mstari wa mbele kupinga” alisema
Alisema tatizo kubwa la ndoa hizo katika Wilaya ya Bahi linasababishwa na mila na desturi za kabla la wagogo ambapo wasichana huolewa wakiwa bado wadogo.
“Sasa hii ya kumuoa mtoto wa miaka 10 ni kiboko maana mtoto mwenyewe hata maziwa hana ana umbo dogo inasikitisha sana” alisema
Alisema tatizo hilo pia limekuwa likichangiwa na mwamko finyu wa elimu kwani wananchi wengi ni wafugaji wanajali zaidi mifugo kuliko binadamu na hata umaskini umekuwa ukichangia.
“Baba ana mtoto wa miaka 10 na anataka kupata fedha akaamua kumuoza binti yake ili apate mbuzi na fedha lakini haangalii madhara ambayo mtoto Yule anaweza kupata.” Alisema.
Hata hivyo mtuhumiwa, Mnamba alisema alilazimishwa ndoa hiyo na bibi wa mtoto aliyetajwa kwa jina la Ntolwa ambaye alisema mtoto huyo ni mkubwa na anaweza ndoa jambo ambalo lilifanya amchukue na kwenda kuishi nae.
“Mimi nilikaa na yule mtoto lakini alikuwa hatoshi, nikaenda nikamwambia bibi namrudisha mtoto kwani hatoshi, nikamrudisha kwa bibi yake lakini bibi akamrudisha tena kwangu” alisema mtuhumiwa

No comments:

Post a Comment