Mila ya kuondoa mikosi 'kitigo' ilivyomsababishia Ukimwi
“NILIPATA maambukizi ya Ukimwi mwaka 1990, nakumbuka baada ya kifo cha mume wangu niliambiwa nirithiwe na mdogo wa mume jambo hilo nililipinga , nduguze wakasema kama sitaki kuolewa lazima uondoe kitigo (mkosi) bila hivyo utaua ukoo mzima huo ukawa ni mwanzo wa safari ndefu katika maisha yangu kwani baada ya muda mfupi nilianza
kudhoofika na baadaye kugundulika ninaishi na VVU”
Maneno hayo yanasemwa na Rukia Issa Majata (59) mkazi wa Sahare Tanga.
Nilimfahamu mwanamke huyu wakati wa kongamano la wanawake Kitaifa
lililofanyika Mkoani Dodoma.Hata nilipomuomba kwa ajili ya kufanya
naye mahojiano hakuwa na shaka.
“Mimi niko tayari wakati wowote na niko tayari kueleza kitu gani
kimenitokea katika maisha yangu ili jamii izidi kuongeza juhudi
kupinga mila potofu wanazofanyiwa wanawake na wakati mwingine zimekuwa
zikigharimu maisha yao” anasema mama huyo.
Akiwa ni mwanaharakati wa masuala ya Ukimwi na hata nyanja za ukatili
wa kijinsia anasema kuwa, aliolewa mwaka 1972 na Denea Mwendo ambaye
kwa sasa ni marehemu.
Anasema kuwa,mume wake alifariki mwaka 1990 na wakati huo tayari
alikuwa na watoto wanane.
Hata hivyo,anasema kuwa,baada ya msiba huo kuisha wana ukoo walikaa na
kuamua aridhiwe na mdogo wa mume wake jambo ambalo hakukubaliana nalo
lakini wakasema kama hataki kurithiwa ni lazima aondoe kitigo (mkosi)
la sivyo atamaliza ukoo mzima.
Anasema kuwa aliambiwa hayo kabla hata hajamaliza eda, japo alikuwa
akikataa lakini alikuwa hana sauti kutokana na wao kuwa wengi na
alitakiwa kutafutwa mwanaume aliyefiwa na mume ambaye alikuwa
hamfahamu
Ndipo ulipofika usiku akasindikizwa na mwanamke moja ambaye hamfahamu
kwa jina na yule bwana wa kwenda kumuondoa kitigo alisindikizwa na
mwanaume mwenzake na walipofika huko wakafanya tendo la ndoa huku wote
wakiwa hawajuani, wakati huo ilikuwa ni saa nne za usiku kwa hiyo
ilikuwa si rahisi kumtambua mtu kutokana na giza lililokuwepo.
Rukia anasema kuwa, baada ya miezi sita akaona afya yake inashuka na
wakati huo ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 1990 ,akaona ni heri akapate
ushauri wa kupima virusi vya Ukimwi.
Baada ya kupima akagundulika kuwa ana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
hali ambayo ilimchanganya lakini akaamua kumshukuru Mungu kwa kila
jambo.
Hata hivyo alipewa rufaa ya kwenda hospitali ya Bombo kwa ajili ya
kupima ini, wingi wa damu na CD4 na baada ya wiki moja alifuatilia
majibu na kuonekana kuwa alikuwa na CD4 1050 jambo ambalo lilifanye
asianze kutumia dawa.
‘Nilipewa mlolongowa chakula ambachokitanisaidia na mambo ambayo
yatafanya nisishushe kinga yangu”anasema
Anasema kuwa mwanaume aliyemfanyia kitigo ndiye atakuwa amemuambukiza
Ukimwi kwani hata marehemu mume wake hakuwahi kuugua ugonjwa huo na
alianza kudhoofika muda mfupi baada ya kubakwa na mwanaume aliyetakiwa
kumuondoa mkosi.
Japokuwa aliamua kumuachia Mungu juu ya maisha yake na kuamua kuishia
kwa masharti aliyokuwa akielekezwa na masdaktari hali ambayo imemfanya
kuwa na afya njema mpaka sasa.
Hata hivyo anasema kuwa, mwaka 2006 alifiwa na binti yake aliyemtaja
kwa jina la Rehema na hapo kinga yake ya mwili ikashuka kutokana na
mshtuko ambao ulifanya ashindwe kula na wakati huo ndiyo alianza
kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV).
Anasema kuwa tangu wakati huo ameendelea kutumia ARV lakini mpaka sasa
CD4 zake ziko1066.
Siri ya mafanikio
Rukia anasema kuwa,ameamua kuwa kioo cha jamii na amekuwa akielimisha
vijana mashuleni na sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye mikutano, warsha
na makongamano endapo atachaguliwa kwani amekuwa hana wasiwasi kabisa.
“Mwaka 1999 nilijitangaza kuwa ninaishi na virusi vya Ukimwi hiyo ni
baada ya kujiunga na Umoja la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi Mkoa
wa Tanga TAPHA+ na baada ya kujitangaza baadhi ya watu waliamini na
wengine hawakuamini lakini nilikuwa nimeondoa mnyororo wa wasiwasi”
anasema
Anasema baada ya kujitangaza kuna watu walikuwa wakimnyooshea vidole
lakini hakujali hilo kwani tayari alikuwa ameenga moyo wa kukubali
kuwa alikuwa akiishi na virusi vya Ukimwi.
Wito kwa jamii
Anasema kuwa,wito wake mkubwa kwa jamii ni kuwa kuona Ukimwi kama
ugonjwa wa kawaida na kujikubali pale unapokuwa umepata maambukizi.
“Ukimwi ni kama mafua watu wote wanakufa na makaburi yanachimbwa kila
siku na wanaokufa na kuzikwa si wote wanaishi na virusi vya Ukimwi,
kwani hata maralia, kisukari, kansa vyote vinaua” anasema
Rukia anasema kuwa wenye virusi vya Ukimwi wanakupa mapema kutokana na
upumbavu wao kwani elimu imesambaa nchi nzima namna ya kujilinda na
hata unapokuwa umeathirika unatakiwa ufanye nini.
Maisha yake ya sasa
Anasema kuwa, kwa sasa maisha yake yana amani zaidi kutokana na
kujikubali na kwa sasa anafanya kazi kama mlinzi katika Shirika la
Tree of Hope ambao walimuwezesha kuja Dodoma kuhudhuria kongamana
laKitaifa la wanawake.
Anasema Tree of Hope walimpa elimu ya ukatili ili aweze kuwasaidia
katika kufanya kazi zao.
Pia anasema kuwa amekuwa akifanya kazi ya kutoa ushauri nasaha katika
baadhi ya hospitali na pia mjasiriamali wa nguo.
Rukia anasema kuwa sasa Mungu amemjalia maisha yake na amani na
anajivunjia wajukuu 11 aliokuwa nao.
Aidha anabainisha kuwa,aliolewa mwaka 2003 na mwanaume ambaye hana
maambukizi ya Ukimwi na wamekuwa wakiishi pamoja moaka sasa.
Anasema kuwa maisha yake ni ya amani na anamshukuru mumewe huyo kwa
kumsaidia kwani mara kadhaa hulazimika kwenda kumchukulia dawa.
“Watu wengine wanasema Rukia ni muongo kaamua tu kula hela kwa
kujitangaza kuwa na virusi” anasema
Rukia ambaye anazifahamu ABC hazi Z za mbinu za kuepukana na Ukimwi
anasemakubwa kuliko zote ni kuacha ngono,kubadili tabia na mapenzi si
lazima kujamiiana.
Anasema kuwa jamii ina nafasi nzuri za kujikinga na maambukizi ya
Ukimwi kwani elimu imekuwa ikitolewa kila kona ya nchi cha muhimu ni
kubadili tabia.
“Nawaambia vijana vyote ving’aavyo si dhahabu vingineni vya kuchovya
kinga ni muhimu” anasema
Pia anazitaja hatua nne za maambukizi kuwa ni pamoja na kipindi cha
kwanza ni kipindi ficho ambapo unaenda kupima baada ya miezi mitatu.
Anasema hatua ya pili unakwenda kupima lakini maambukizi hakuna wala
huumwi na huna tatizololote.
Hatua ya tatu ni utata mwambata huwa ni kipindi cha utatanishi unakuwa
na magonjwa nyemelezi mara mkanda wa Jeshi, mara kifua kikuu,homa
haziishi, majipu lakini vitu kama hivyo ukienda hospitali unapona
Rukia anasema kuwa hatua ya nne ni kipindi tuli ukidharau kutumia
dawa au kuamua kwenda kwa waganga wa kienyeji unakwenda moja kwa moja
kwenye Ukimwi.
Anasema kuwa ukifikia katika hatua hiyo dawa ni maombi, faraja na
paracetamol hapo unakuwa umefika wakati wako wa kufa.
Aidha Rukia anakumbuka mwanamke aliyemsindikiza kufaniwa kitigo
alifariki mwaka 2000 na kitigo hicho alifanyiwa katika Kijiji cha Mtakuja.
No comments:
Post a Comment