Sunday, April 13, 2014

Ukatili wa kijinsia ulivyoharibu ndoto za Felista


Na Mwandishi wetu
UKATILI wa Kijinsia ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakiathiri maendeleo ya wanawake. Kumekuwa na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali na hata yale ya kimataifa kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa katika jamii.
Takwimu zinaonesha kuwa, ukatili wa wanawake majumbani umeendelea kuongezeka, kati ya wanawake watatu, wawili wamefanyiwa vitendo vya ukatili.
Asilimia 39 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili na asilimia 20 ya wanawake wamewahi kufanyiwa ukatili wa kingono.
Pia takwimu zinaonesha kuwa asilimia 45 ya wanawake wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na takribani wasichana watatu kati ya 10 wametendewa angalau tendo moja la ukatili wa kijinsia kabla ya kufikisha iaka 18.
Felister John  (30),mkazi wa Ruamlimi Wilaya ya Musoma Mkoani Mara ni miongoni mwa wanawake waliowahi kukutana na vitendo vya ukatili wa kijinsia. Mwanamke huyo ambaye sasa ni maarufu kutokana na kazi yake ya kuuuza mboga mboga anasema kuwa, aliolewa mwaka mwaka 2001 akiwa na umri wa miaka16 baada ya kumaliza elimu ya msingi.
Nilikutana na Felister wakati wa Kongamano la Kitaifa la wanawake lililoandaliwa na Muunganio wa asasi zinazoshughulikia masuala na kijinsia lililomalizika hivi karibuni mkoani Dodoma.
Licha ya ucheshi wake lakini ni mwenye historia ndefu katika maisha yake ambapo wakati mwingine unaweza kuona hailingani na umri wake.
Kulingana na Felista siku chache baada ya kufunga ndoa  wakaenda kijijini kwa mumewe Tarime  kusalimia na kufikia kwa shemeji yake ambaye ni kaka wa mume wake .
Cha ajabu shemeji yake akaanza kumtaka kimapenzi  jambo ambalo hakukubaliana nalo na huo ukawa mwanzo wa kufanyiwa visa na kuna siku aliwahi kumtamkia kuwa kuna kitu kibaya atamfanyia kwani yeye ni muolewaji tu.
Baada ya muda akaanza kuugua kichomi, ndipo shemeji yake aliposema kuwa anataka amtengenezee dawa lakini cha kushangaza dawa ilikuwa ni pilipili iliyokuwa imesagwa.
 “Shemeji aliweka mkaa kwenye sufuria , moto ulikuwa mkali, nikakalishwa chini nikaambiwa nipanue mguu wakaweka moto chini ya miguu na kisha nikafunikwa na shuka na  blanketi wakaja watu wakashikilia zile nguo nilizofunikwa ili hewa isiingie wala kutoka na akawekwa pilipili kwenye moto zile pilipili zilipokuwa zikiungua harufu ilikuwa kali nikaanza kushindwa kupumua” anasema
Anasema kuwa, alipofunuliwa nguo alizokuwa amefunikwa ambazo ni blanketi na shuka alikuwa hajiwezi kabisa na tayari alikuwa amejisaidia haja ndogo na alikaa kitandani siku tatu bila kutoka nje.
Shemeji yake akamuambia hiyo dawa inatakiwa irudiwe baada ya siku tatu,lakini alikataa kata kata.
“Kwa kweli sikukubali akaenda kunishtakiwa kwa mume wangu kuwa nilikuwa nikikataa na mume wangu akaungana na kaka yake kuwa ni lazima nitumie dawa ili nipone, niliamua kukimbia lakini mume wangu alinikimbiza  hadi kunikamata na kwa kushirikiana walifanikiwa kunifunika na kuniwekea tena ile dawa nikaanza kulia kuwa ninaungua mapaja wakasema acha niungue kwani walikuwa wakinitengeneza dawa” anasema
Baada yakuachiwa kutoka kwenye nguo alizokuwa amefunikwa mguu ulikuwa umeungua vibaya akawa na maumivu makali sana hali iliyosababisha kupoteza fahamu.
Hata hivyo baada ya fahamu kumrudia aligundua amejisaidia haja ndogo na kwa vile walikuwa wamembananisha mguu gamba la mguu wa kulia likabaki mguu wa kushoto na kufanya pale palipobanduka kuwa na kidonda kikubwa.
“Nikaugua mwezi mzima hakuna wa kunipelekahospitali,siwezi kutembea wala kunyanyuka najisaidia humo humo ndani  ikafikia hatua mguu ukanuka wakaniletea manyoya ya sungura na asali wakaniwekea kwenye mguu ulioungua wakasema hakuna kuosha mguu” anasema
Felista anasema kuwa,baada ya wiki mbili mguu ukawa umeoza anakumbukailikuwa ni Agosti 3, mwaka 2001 akawa mtu wa ndani tu manyoya ya Sungura aliyowekewa yalikuwa palepale lakini nyama za miguu zikawa zikidondoka chinikutokana na kuoza.
  “Nikafikiria nifanye nini nikapata wazo la kuandika barua ili ndugu zangu wapate taarifa, lakini nilipokuwa naandika barua shemeji akanikuta akachukua barua ile na kuichana nililia sana maana sikujua hatma yangu itakuwa nini” anasema

Hata hivyo akapata wazolingine la kumtuma kijana wa jirani kwenda stendi amtafute ndugu yake aitwaye Mashaka  ili aweze kuwapatia taarifa nyumbani na kwa bahati nzuri aliweza kuwapatia taarifa wakamtuma bibi mzaa mama akafika
Anasema kuwa,bibi yake alipofika alikuta akiwa na hali mbaya na wakati huo alikuwa na mimba ya miezi saba na baadaye ikaamuliwa apelekwe kijijini kwa mumewe  kule Matongo na baada ya kufika huko kikao kilikaa na kukubaliana apelekwe hospitali ya Bugando bili akakatwe mguu lakini hata hivyo kaka yake Wambura Mwikwabe ambaye anaishi Musoma alikataa.
“Wakanipeleka Musoma kwa kaka yangu nikaanza kuhudumiwa na hali yangu ikawa nzuri na siku ambayo uchungu uliponianza nikaenda hospitali na mama mkwe wangu lakini cha kushangaza aliniambia siumwi bali nilikuwa nimetamani vitanda vya hospitali jinsi vilivyokuwa vimetandikwa na kama nina uchungu mbona sioneshi dalili” anasema
Felista anasema kuwa,alijifungua siku hiyo hiyo yaani Oktoba 21, mwaka 2001 na kupata mtoto wa kike na mama yake mzazi alifika na kumhudumia  na baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali akarudishwa tena nyumbani kwa mumewe huku akiendelea kuishi kwa manyanyaso ikafikia hatua anarudi nyumbani kwao na kisha kwa mumewe.
Anasema kuwa mtoto wake wa kike aliyejifungua kwa bahati mbaya  alifariki wakati akiwa na umri wa miezi tisa na alipobeba mimba nyingine kuna siku mumewe alimpiga na mimba hiyo kutoka.
Hata hivyo tayari ana watoto wengine watatu Anna mwenye umri wa miaka tisa anayesoma shule ya Msingi Nyakato akifuatiwa na Ayub na Zacharia ambao bado wako chekechea.
Felista anasema kuwa mwaka 2012 likazuka jambo jipya.dada yake alikuwa amelazwa hospitali na hilo likamlazimu kuchukua watoto wa dada yake na kuishi na pale nyumbani.
Jambo hilolikamkera mumewe ambaye aliwafukuza watoto hao wakati akiwa hospitalini akimuangalia mgonjwa.
“Baada ya kurudi sikuwakuta watoto wa dada, nilipomuuliza mume wangu aliniambia kuwa watoto wale wana baba na mama na hawahitaji nyumbani pale,nilishangaa kwa vile pale nyumbani kulikuwa na mama mkwe na watoto watano na ndugu wa mume wangu,nikamwambia kama wale umewafukuza basi  na hao wa ndugu wako nao waondoke kwani mtoa matumizi alikuwa ni mimi na siko tayari kutoa matumizi tena, ukawa ugomvi mkubwa” anasema
Anasema kuwa ugomvi huo ukaingiliwa na ndugu wa mumewe akiwemo wifi yake Sophia ambao walikaa kikao na kuamua kumfukuza
“Nilikataa kuondoka kwa vile nyumba ile nilikuwa nimejenga mimi na kiwanja ambacho tumejenga nyumba nilinunua mwenyewe kwa Shilingi 250,000  kutoka kwa Sophia “ anasema
Anasema kuwa, fedha za kiwanja alitoa na kumpa mumewe ili akalipie kiwanja hicho ambapo hata aliporudi na kuuliza kama kulikuwa na kuandikishiana kwa ajili ya ushahidi mumewe alimuambia kwa vile walikuwa ndugu hakuna sababu ya kuandikishiana.
“Baada ya kununua kiwanja hicho tulijenga nyumba ya matofali mabichi lakini ikabomoka na mvua na mara ya pili tukajenga ya tofali za kuchoma vyumba viwili na sebule.” anasema
Felista anakumbuka Julai 21, mwaka jana, mumewe alimpiga hadi kwenda kulazwa wodini kwa siku tatu na wakati akiwa hospitali wifi yake alitafuta gari na kutoa vitu vyote vya ndani na fedha taslimu Shilingi milioni 1.3 lakini hata hivyo majirani wakapinga vitu hivyo kuondoka.
“Nilipopata taarifa nikaenda nyumbani nikakuta Toyota Hiace iko nje wanapakia vyombo na vitanda,nikapiga yowe nikalala chini ili gari lisiondoke dereva alipotaka kuondoa gari  nikamwambia uniue  hapa hapa siondoki” anasema
Anasema kuwa alipata ujasiri wa kupiga simu kwenye Shirika la ABC Foundation ili kupata masaada kwani wana kitengo cha kutetea haki za wanawake na watoto na wao wakapiga simu polisi,mara polisi wakafika na kukuta baadhi ya watu wakishikiliwa na wananchi.
Miongoni waliokuwa wakishikiliwa ni Sophia, mdogo wa mume wangu aitwaye Paul pamoja na mama mkwe.
Hata hivyo  mume wa Sophia  alifanikiwa kukimbia na alipoingia chumbani alikuta fedha alizokuwa amehifadhi hazipo.
Polisi wakaamua vyombo hivyo vishushwe na watuhumiwa walifikishwa kituo cha polisi na wakafunguliwa mashaka.
Lakini watuhumiwa walikuwa wakicheleweswa kufikishwa mahakamani  lakini Agosti 3, mwaka jana walifikishwa mahakama ya mwanzo Kitaji,Musoma.
Anasema kuwa kabla ya kufikishwa mahakamani watuhumiwa hao polisi walikuwa wakimzungusha na hapo aliamua kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya kuomba msaada jambo lililowachukiza askari na kusema kuwa alikuwa akiwachongea kwa bosi wao kwani walikuwa wamemuambia alete shahidi ili kesi iende Mahakama ya Wilaya.
Tangu kesi imefunguliwa mashahidi wamekuwa wakizungushwa kilawakienda kesi inaahirishwa,.
“Lakini naamini mahakama itatenda haki kwani nyumba ile ni yangu na hata fedha walizochukua naomba Mungu warudishe kwani nilikuwa nikidunduliza muda mrefu kutokana na biashara yangu ya kuuza mboga mboga” anasema
 Anasema kuwa mumewe tangu ampige na kukimbilia Tarime kwa kaka yake Julai mwaka jana, mpaka sasa bado hajarudi na amekuwa akilea watoto peke yake.
Felista anataka wanawake kuvunja ukimya pindi wanapofanyiwa mambo ya ukatili kwani ukatili umekuwa wakati mwingine ukikatisha uhai na hata kusababisha vilema vya maisha.
“Wanawake wasikae kimya wanapofanyiwa ukatili, wawe wazi ili waweze kusaidiwa,mimi naona kama nilikosea kuolewa na mwanaume yule kwani mara kadhaa nimenusurika kupoteza maisha kutokana na kipigo” anasema
Anasema kuwalicha ya kufanyiwa ukatili mara kadhaa ikiwemo kuchomwa moto, kupigwa hadi mimba kutoka na hata kutaka kudhulimiwa nyumba lakini ameendelea kufanya shughuli zake kama kawaida kutokana na kutokaa kimya kwani matukio mengi ya ukatili aliyokuwa akifanyiwa amekuwa akitoataarifa hali ambayo mara nyingi hata majirani wamekuwawakimtetea pindi wanapoona kuwa haki haikutendeka.

Mguu wa Felista unavyoonekana kwa sasa baada ya kupona


2.Felista akizungumza wakati wa kongamano la kitaifa la wanawake lililofanyika Mjini Dodoma.




No comments:

Post a Comment