Sunday, April 13, 2014

Safari bado ndefu kufikia usawa wa kijinsia


Na Mwandishi Wetu
“LAZIMA wanawake wajengewe uwezo tunataka nchi inayojali usawa wa kijinsia, hatutaki kusikia maneno ya kejeli kwa wanawake wanaojitokeza kugombea uongozi kwa  lengo la kuwavunja moyo ili warudi nyuma”
Maneno hayo yanasemwa na mwanasiasa Mkongwe na Mbunge wa viti maalum Anna Abdallah wakati wa mkutano wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa nchini (Ulingo) uliofanyika Mjini Dodoma.
Anabainisha kuna umuhimu kwa vyama vya siasa kuwa na demokrasia ya kweli kwani bila kufanya hivyo mfumo wake wa uendeshaji kamwe hauwezi kujali usawa wa kijinsia.
Kulingana na Abdallah vyama vingi vya siasa havina usawa wa kijinsia jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi. Pamoja na hayo anasema  ataendelea kukemea vitendo vya kudhalilisha wanawake wanaotafuta uongozi.
Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa Ulingo anasema ataendelea kuwa mkali kuona wanawake wanaotafuta uongozi
wanapodhalilishwa  kwani wengi wao wamekuwa wakinyanyasika kwa kauli chafu na maneno ya kejeli kuwa hawawezi uongozi.
"  Ndani ya siasa wanawake wananyanyasika hasa pale wanapotafuta uongozi, utasikia mtu anasema wewe utamchaguaje mwanamke ambaye
anachuchumaa wakati wa kwenda haja, haya si maneno mazuri mtu wa namna hiyo anamdharau mwanamke ambaye ni sawa na mama yake mzazi " anasema

Kulingana na mwanasiasa huyo wanataka kuweka wazi kuwa mwanamke ana nafasi waheshimiwe kwani hata vijana wamekuwa na misemo ya ovyo juu ya wanawake wakati wamezaliwa na wanawake hao hao ambao wanawakosea adabu.
Anasema kuna haja ya kuwajengea uwezo wanawake waonekane wana uwezosawa na wanaume na kuondoa misemo ya ovyo.
“Tunapopata nafasi lazima tuelezane na tujengeane uwezo  wanawake wana fursa, nia na uwezo hasa pale wanapochaguliwa kuwa viongozi” anasema
Anabainisha kuwa bunge la sasa la katiba lina wajumbe zaidi ya 600 ambapo wajumbe 201  wanatoka maeneo mbalimbali na sasa kinachofanyika ni kuwajengea uwezo wanawake ili watakapokwenda kwenye kamati wapate
kuwasemea wanawake wenzao.
"Lazima tuelezane na kujengeana uwezo tunataka nchi  inayotetea usawawa kijinsa  lazima ifike wakati ionekane kila mtu ana thamani sawa" anasema
Aidha maslahi ya wanawake wa Tanzania  yanaendana na uwazi na hapendi kuona kunakuwa na udhalilishaji ua utoaji wa maneno machafu kwa wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali
Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo(Chadema) anataka wanawake walio bungeni kuwaunga mkono na kuwachagua wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali .
Pia katika rasimu ya kwanza amani ilikuwa ni moja ya tunu ya taifa lakini katika rasimu ya pili tunu hiyo haipo na wana jukumu la kuhakikisha tunu ya amani inarudi ili kwenda sambamba na mambo mengine.
Anataka Ulingo kusimama na kukemea hasa pale ambapo wanaona mwanamke anadhalilishwa, hata anapofanyiwa hivyo na vyombo vya habari.
Aidha ,Mbunge wa viti maalum, Margareth Sitta anasema mpaka sasa Tanzania imeshindwa kurudisha shuleni wanafunzi wanaopata mimba ili waendelee na masomo pindi wanapojifungua.
"Tunapoteza wasichana wenye uwezo mkubwa, Nchini Kenya Mwanafunzi
anapojifungua anaruhusiwa kuendelea na masomo hapa Tanzania kuna nini?" anasema
Alitaka katiba iwe na kipengele cha kurudisha tena kwenye masomo
wanafunzi wanaopata ujauzito.
"Tuongeze kipengele hicho kwenye katiba hiii ili wanafunzii wanaopata
mimba waendelee na masomo.
Victoria  Lihiru kutoka Ulingo anasema  mchakato wa katiba haukusahau wanawake  kutokana na kujitokeza kwa masuala mengi ya kijinsia.
Anasema rasimu ya pili imeweka wazi kuwa wanawake wote ni sawa.
"Kwenye tunu za taifa, amani haijatajwa ,usawa wa kijinsia haujatajwa ni suala la kupigia kelele ili vitu hivyo virudi" anasema
Anabainisha kuwa haki za wanawake zipo lakini hakuna tume ya kusimamia utekelezaji wake kwani katiba ni kitu kimoja na utekelezaji ni kitu kingine.
Pia haki za wanawake wenye ulemavu pia zimekosekana kwenye
rasimu ya pili ambayo pia haijasema haijasema nani ni mtoto kama ni miaka 18 au 21 katiba ni lazima iainishe mtoto ni nani.
"Hata vyama vya siasa havijabanwa kuzingatia masuala ya kjinsia pia
katika suala la kufanya maamuzi katiba imebaki kimya.Katika nchi
nyingine  kuna bajeti katika masuala ya kijinsia yamekuwa yakitengewa bajeti na hivyo kurahisisha  utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali.
Aidha Mjumbe wa Bunge la katiba, Dk.Ave Maria Semakafu anataka kuwe na tume ya kufuatilia masuala ya usawa wa kijinsia ambapo Stella Jairos kutoka Sauti ya Wanawake wenye ulemavu Tanzania anasema walemavu ni kundi pekee la unyonge ambalo huwezi kukwepa  ukweli uliopo.
Pia anasema elimu  ni chanzo cha maarifa yote vilevile ni chanzo cha kila jambo wanawake wenye ulemavu wafikiriwe kupewa nafasi za bure katika shule za msingi na sekondari ili kuongeza idadi ya wanawake wanaopata elimu ambayo itawasaidia katika maisha yao.
Vilevile anataka walemavu wathaminiwe katika suala la usalama wa uzazi.
Pamoja na hayo hata katika masuala ya kodi yaangaliwe kwani walemavu wasioona wamekuwa  wakiingia gharama mara mbili kutokana na kulipa watu wanaowaangoza wakati kiwango cha malipo wanayofanyia kazi yakikatwa kodi na kupungua hali inayofanya maisha kwao kuwa magumu.
Jairos anasema katika rasimu ya pili kulikuwa hakuna makala za kutosha .
“Shirika la Oxfam lilifadhili nakala 50 nchi nzima watu wengi wenye ulemavu rasimu ya pili hawaijui” anasema
Mbunge wa Kasulu Vijijini, kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi ,Agripina Buyogera  anasema sasa wanawake wamebadilika na kuwa na mshikamano sana.
Anasema alisimama na kugombea Ubunge kupitia jimbo na alifanikiwa kuchaguliwa anaamini kama wakiingia 50/50 wanawake wanaweza.
Pia Mbunge huyo anasema sasa anasoma elimu ya sekondarii ili aweze kupata cheti cha kidato cha nne kwani wakati akichaguliwa kuwa Mbunge alikuwa na elimu ya darasa la saba na anajiendeleza ili aweze kuwa na sifa za kugombea nafasi hiyo tena.
“Kutokana na umaskini sikubahatika kupata elimu nikachaguliwa kuwa Mbunge nikiwa na elimu ya darasa la saba na sasa najiendeleza, wanawake wanaweza” anasema
Anasema vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na udhalilishaji vimekuwa vikitokea mara kwa mara kuna wakati wanaona wanawake wananyanyaswa na kubughudhiwa wajitahidi na kujenga ushujaa wa kujiamini.
 
Mwanasiasa Mkongwe Nchini, Anna Abdalah











No comments:

Post a Comment