JESHI
la Polisi Mkoani Dodoma linamshikilia daktari feki mkazi wa Katesh Wilaya ya
Kiteto Mkoa wa Manyara, Mohamed Abdallah (35), pichani baada ya kukutwa akitoa
huduma ya matibabu bila kuwa na kibali wala leseni.
Hadi
anakamatwa tayari alikuwa ametoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 20.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio hilo lilitokea Agosti 12,
mwaka huu majira ya saa tisa mchana katika Kijiji cha Nyerere Kata ya
Hogoro, Tarafa ya Zoissa Wilaya ya Kongwa,.
Alisema
mtu huyo alikutwa akitoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 20 huku
akiwa hana kibali wala leseni ya kutoa huduma hiyo.
Kamanda
Misime alisema baada ya taarifa za siri kulifikia Jeshi la Polisi, mtuhumiwa
alikamatwa katika nyumba ambayo haistahili kufanyiwa shughuli za matibabu
ambayo ni mali ya Sikitu Magomba ambapo mtuhumiwa alipanga katika kijiji hicho
cha Nyerere.
Alisema
baada ya mtuhumiwa kupekuliwa alikutwa na dawa za aina mbalimbali zenye nembo
ya MSD, Drip 500mls chupa tisa ambazo haziruhusiwi kuuzwa, sindano na baadhi ya
vifaa tiba vidhaniwavyo vilipatikana kwa njia isiyo halali.
![]() |
| Baadhi ya dawa na vifaa tiba vilivyokutwa |
Aidha
baada ya kuhojiwa mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo na kwamba hana taaluma
yoyote ya utabibu na elimu yake ni darasa la saba.
Alisema
uchunguzi zaidi unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Kamanda
Misime alitoa wito kwa wananchi kuwa makini na kuhakikisha wanatibiwa kwenye
Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali zinazofahamika ili kuepuka madhara dhidi
ya tiba bandia.
Pia
alitaka wananchi kuwafichua madaktari feki ili waweze kuchukuliwa hatua
za kisheria kwani unapotibiwa na mtu ambaye hana Utaalam kama Daktari mbali ya
kuumwa kwanza hutapona na pili utapata madhara ambayo yanaweza kukuletea
madhara ya kudumu na pengine kupoteza maisha.






