Saturday, August 15, 2015

huyu ndiye daktari feki aliyenaswa dodoma



JESHI la Polisi Mkoani Dodoma linamshikilia daktari feki mkazi wa Katesh Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara, Mohamed  Abdallah (35), pichani baada ya kukutwa akitoa huduma ya matibabu bila kuwa na kibali wala leseni.
Hadi anakamatwa tayari alikuwa ametoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 20.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio hilo lilitokea Agosti 12, mwaka huu  majira ya saa tisa mchana katika Kijiji cha Nyerere Kata ya Hogoro, Tarafa ya Zoissa Wilaya ya Kongwa,.
Alisema mtu huyo alikutwa akitoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 20  huku akiwa hana kibali wala leseni ya kutoa huduma hiyo.
Kamanda Misime alisema baada ya taarifa za siri kulifikia Jeshi la Polisi, mtuhumiwa alikamatwa katika nyumba ambayo haistahili kufanyiwa shughuli za matibabu ambayo ni mali ya Sikitu Magomba ambapo mtuhumiwa alipanga katika kijiji hicho  cha Nyerere.
Alisema baada ya mtuhumiwa kupekuliwa alikutwa na dawa za aina mbalimbali zenye nembo ya MSD, Drip 500mls chupa tisa ambazo haziruhusiwi kuuzwa, sindano na baadhi ya vifaa tiba vidhaniwavyo vilipatikana kwa njia isiyo halali. 
 
nyumba aliyoitumia

Baadhi ya dawa na vifaa tiba vilivyokutwa

Aidha baada ya kuhojiwa mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo na kwamba hana taaluma yoyote ya utabibu na elimu yake ni darasa la saba.
 Alisema uchunguzi zaidi unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani. 
Kamanda Misime alitoa wito kwa wananchi kuwa makini na kuhakikisha wanatibiwa kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali zinazofahamika ili kuepuka madhara dhidi ya tiba bandia.
Pia  alitaka wananchi kuwafichua madaktari feki ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwani unapotibiwa na mtu ambaye hana Utaalam kama Daktari mbali ya kuumwa kwanza hutapona na pili utapata madhara ambayo yanaweza kukuletea madhara ya kudumu na pengine kupoteza maisha.


No comments:

Post a Comment