Friday, December 27, 2013

Kutana na mzee nzije shanga komite mwenye wake 12 na watoto 52..afanya mabadiliko ya maisha

KUISHI na wake wengi si kazi rahisi na sasa sina nguvu nazeeka, sitaoa tena wanawake nilionao wanatosha”.
Nzije Shanga Komite

Maneno hayo yanasemwa na mfugaji wa kabila la Kimasai, Nzije Shanga Komite  mkazi wa Kijiji cha Mkakatika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambaye ana wake 12 na watoto 52. Alipoulizwa na mwandishi wa makala haya idadi ya watoto aliyonayo alisema hafahamu lakini mtoto mkubwa wa mzee huyo anasema wako watoto 52 katika familia hiyo wakiwemo wa kike 30 na wa kiume 22.
“Nina wake 12, watoto wengi wengi hata majina siwakumbuki na wengine wamepata wenzao wanajitegemea,” anasema mzee huyo. Mfugaji huyo ambaye amepanga ratiba ya kulala na kila mke wake, anasema kuishi na wake wengi si rahisi kwani kuna wakati huwa anachoka na kutaka kupumzika.
Mzee huyo akiwa ni kati ya wafugaji 68 wa Wilaya ya Bahi walioamua kubadilika na kuvuna mifugo yao ili kuwa na maisha ya kisasa. Kwa mujibu wa Mzee huyo anasema alizaliwa mwaka 1955 kijijini hapo ambapo wazazi wake walikuwa wafugaji na hakupata muda wa kwenda shule kutokana na kufanya kazi ya kuchunga mifugo ya baba yake ambapo maisha yao yalikuwa ya kuhamahama kutafuta malisho.
Mzee Nzije anasema mke wake wa kwanza alimuoa mwaka 1979. Mwanamke huyo ambaye alifanikiwa kuzaa naye watoto sita alifariki mwaka jana na kuzikwa kwenye boma la nyumba yake. Mtoto wake wa kwanza alizaliwa mwaka 1984 na tangu wakati huo amekuwa akioa mfululizo, wakati mwingine wake wawili au watatu kwa mwaka moja hadi walipofikia wake 12.
Pia mke wa mwisho alimuoa mwaka 2007 ambaye anaitwa Gasi na wanaishi wote mpaka leo, lakini hajafanikiwa kupata mtoto. Amekuwa akiwahudumia wanawake hao kwa mavazi, malazi, chakula na matibabu pindi wanapougua. Anakumbuka mkewe wa kwanza ambaye kwa sasa ni marehemu alimuoa kwa mahari ya ng’ombe 27 na mkewe wa mwisho alimuoa kwa mahari ya ng’ombe 12.
Amekuwa akiwapangia zamu wanawake hao kwa ajili ya kulala nao ambapo kwa mwanamke moja amekuwa akikaa kwa siku tatu au nne kisha kwenda kwa mwanamke mwingine. “Kuna wakati huwa nachoka na huwa nawaambia sitaki kabisa nimechoka siwezi kufanya kitu,” anasema.
Anaona kadiri siku zinavyokwenda anazidi kuwa na umri mkubwa na hivyo si rahisi tena kushiriki mapenzi na wake zake kila mara. Hata hivyo, kulingana na mila za Kimasai mwanamke anapokuwa na ujauzito hadi kujifungua anatakiwa kukaa miaka miwili bila kukutana na mwanamume. “Hata unapokwenda kumgusa anakataa anasema anaweza kuharibu mtoto wake,” anasema.
Alipoulizwa amekuwa akifuata njia za uzazi wa mpango alisema, wake zake hawatumii njia za uzazi wa mpango bali wamekuwa wakifuata mila zao kwa kusubiri miaka miwili tangu ajifungue na hata baada ya mtoto kuacha kunyonya ndipo anaweza kukutana na mumewe.
“Hawatumii uzazi wa mpango wanarekebisha wenyewe huwa wanajua siku zao za hatari hata akipata ujauzito anakaa mpaka ajifungue na anakuwa mpweke kwa miaka miwili hadi akimwachisha mtoto kunyonya hapo anaruhusiwa kuendelea na tendo la ndoa,” anasema.
Akielezea manufaa aliyopata tangu aanze kuvuna mifugo ni pamoja na kununua gari la kutembelea, kujenga nyumba ya kulala wageni Bahi Mjini, kununua trekta la kisasa na pia ameweza kununua kiwanja Bahi Mjini ambapo anatarajia kujenga nyumba ya kisasa ambayo ataishi na familia yake.
Hata hivyo anasema ukame umekuwa na athari kubwa kwa mifugo yake kutokana na mwaka jana ng’ombe wake 1,800 kufa kutokana na ukame wa kutisha ulioikumba Wilaya ya Bahi. Mbali na hayo anasema amenunua trekta ili aendeshe kilimo cha kisasa ambapo mwaka huu anatarajia kulima ekari 70 za mahindi, mtama na ufuta.
sehemu ya familia

Aidha, maji kwa ajili ya kunywesha mifugo yamekuwa tabu, lakini wanahangaika kwa kuhamisha hamisha mifugo ambapo sasa ana ng’ombe wanaokaribia 1,000 ambao amewagawa katika makundi. Mzee huyo, hivi karibuni alikabidhiwa ramani ya nyumba na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa makazi bora kutokana na kuhamasika na kuamua kuuza baadhi ya mifugo yake ili aweze kujenga makazi bora.
Lakini bado hajaanza ujenzi huo kutokana kutafuta fedha za kumaliza kulipa mkopo wa trekta ambapo sasa anadaiwa Sh milioni 27. Pia alikopa trekta hilo pamoja na jembe lake ambapo trekta pekee lilikuwa likiuzwa kwa Sh milioni 32 na ameshalipa milioni 11. Mbali na hilo Mzee huyo amechangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Kidete.
Kulingana na mzee huyo changamoto kubwa ni uhaba wa maji, lakini anafanya juhudi kuhakikisha anatafuta wataalamu ili aweze kuchimba kisima. Pamoja na hayo anachotamani sasa ni kuchimba kisima ambacho kitaondoa adha ya upatikanaji wa maji katika familia yake na hata kwa ajili ya kunywesha idadi kubwa ya mifugo aliyonayo.
Anabainisha kuwa amebadili mawazo na sasa nyumba ya kisasa anayotaka kuijenga kijijini Mkakatika sasa ataijenga Bahi Mjini baada ya kununua kiwanja kikubwa. Nyumba ya kisasa anayotaka kuijenga itakuwa na vyumba nane na sebule ambapo anataka iwe nyumba bora ya mfano kwa wafugaji wengine.
Aidha anachosubiri ni kupata hati, kuchora ramani ili ujenzi uanze, lakini anategemea kuanza baada ya msimu wa kilimo kwani anatarajia mazao atakayopata akiuza fedha zitakazopatikana ndizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Mmoja wa wake wa mzee huyo, Eva Ishando (29) anasema ni mke wa mzee huyo, lakini hakumbuki aliolewa akiwa mke wa ngapi ila anachokumbuka aliolewa mwaka 2004.
Mama huyo mwenye watoto watatu anasema mtoto wa kwanza na wa pili alijifungulia katika Kituo cha Afya cha Bahi, lakini mtoto wa tatu alijifungulia nyumbani kutokana na kupata uchungu akiwa bado nyumbani. “Nilichelewa na muda ulifika nikiwa nyumbani wenzangu walinisaidia nikajifungua,” anasema.
Umbali uliopo kijijini wanapoishi hadi hospitali imekuwa changamoto kubwa kwani hata mtoto anapozaliwa kufuatilia chanjo za kliniki imekuwa ni kazi ngumu. Pia anaitaja changamoto nyingine ni upatikanaji wa maji ambapo wamekuwa wakichota maji umbali wa kilomita 20 kutoka wanapoishi kwenye Kijiji cha Ugimaa.
“Shule, hospitali na hata tunakochota maji ni mbali, maji tumekuwa tukichota kwa kutumia punda,” anasema. Mke mwingine wa mzee huyo ni Gaudencia Nzije (45) ambaye ana watoto saba. Anasema maisha ya kijijini si rahisi kwani huduma muhimu zimekuwa zikipatikana umbali mrefu, lakini hata hivyo pindi wanapougua mumewe hutafuta usafiri kwa ajili ya kuwafikisha hospitali.
Kwa upande wake, Kezia Nzije akiwa kati ya wake wa mzee huyo ambaye kwa umri anaonekana mdogo anasema hakumbuki alizaliwa mwaka gani, lakini amezaa na mzee huyo mtoto moja ambaye kwa sasa ana umri wa miezi saba, anataja jina la mtoto huyo kuwa ni Kilaita. “Mtoto huyu nilimzaa Mei mwaka huu na nilijifungulia nyumbani,” anasema.
sehemu ya familia

Mmoja wa watoto wa mzee huyo Mafanya Nzije (12), anayesoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Lowassa kijijini hapo anasema anaona maisha ya nyumbani hapo ni ya kawaida kwani amekuwa akihudhuria shule na anataka kusoma hadi amalize darasa la saba.
Kwa upande wake mzee huyo ambaye ni mmoja wa wafugaji 68 wa Wilaya ya Bahi walioamua kubadilika ili waweze kuishi maisha ya kisasa kwa kuvuna mifugo yao, anasema hakubahatika kupata elimu na alipokuwa mdogo alikuwa akichunga mifugo ya baba yake jambo lililofanya kukosa fursa ya kupata elimu.
Anasema anafurahia maisha anayoishi baada ya kuamua kubadilika ambapo aliuza baadhi ya mifugo yake na kununua gari kwa ajili ya kutembelea na sasa amefungua nyumba ya kulala wageni ambayo pia ina biashara ya baa Bahi Mjini. Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa anasema sasa amejizatiti kuhakikisha wanafikia wafugaji wengi ili wapate elimu na hatimaye kuvuna mifugo ili waweze kuwa na makazi bora.
Alisema katika wilaya hiyo kuna wafugaji wenye ng’ombe wengi wanaoishi maisha yasiyo bora wakati wanaweza kupunguza mifugo hiyo kwa kuuza na kupata fedha za ujenzi wa makazi bora na hata kupeleka watoto wao shuleni. Anasema katika mpango huo wa kuhamasisha wafugaji kuwa na makazi bora wamefanikiwa kwani mzee huyo sasa ameweza kujenga nyumba ya kulala wageni ambayo pia imetoa ajira wa wananchi wengine.
Akiwa na mkuu wa mkoa

Mkuu wa mkoa Dk Nchimbi akionesha ramani ya makazi ya Mzee

Mkwasa anasema waliamua kumtengenezea mzee huyo ramani kwa ajili ya kuboresha makazi yake kutokana na kuwa ni mkulima na mfugaji mkubwa, lakini anaishi kwenye nyumba ya tembe. Mkwasa anasema mzee huyo pia alihamasishwa kuingia katika kilimo bora na cha kisasa na sasa amefanikiwa kununua trekta ambalo litamsaidia katika shughuli mbalimbali.
“Mzee Nzije ni mpenda maendeleo najitahidi kumbadilisha awe mfugaji wa mfano yaani kufuga kisasa na kilimo ndiyo maana nilimsimamia akopeshwe trekta,” anasema Mkwasa. Anasema anataka mfugaji huyo awe mfano katika elimu hasa kusomesha watoto wake vizuri ili wafike mbali.
Imetoka kwa mara ya kwanza Nyota habarileoJumapili

Monday, December 23, 2013

Chama cha Waandishi Dodoma chakabidhiwa kompyuta tatu


KAMPUNI ya simu  ya Vodacom imekabidhi kompyuta tatu na mtambo wa kuunganisha kompyuta kwa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (CPC)  vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 5.3
Mwakilishi wa kampuni hiyo, Salum Mzee amesema  kompyuta hizo zimetolewa ili kutimiza ahadi waliyoitoa na kutaka vifaa hivyo kutumika kwa ajili ya kusaidia kazi za uandishi wa habari Mkoani Dodoma
Amesema Vodacom  inatambua mchango wa waandishi wa habari kwa kutoa taarifa ambazo zimekuwa zikifikia jamii ambao ndiyo walengwa.

Mwakilishi huyo wa Vodacom amesema mwaka jana walipitisha mpango maalum wa kusaidia vyama vya waandishi wa habari ambapo Sh. Milioni 40 zilitengwa na hadi  sasa mikoa iliyofaidika ni pamoja na Tanga, Kagera, Iringa na Dodoma
Pia ameitaka CPC kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika  kwa shughuli iliyokusudiwa ya kuanzia mradi wa internet.
Mgeni rasmi katika makabidhiano hayo Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally alitaka vifaa hivyo vitunzwe vizuri ili viweze kutumika kwa muda mrefu.


Mwakilishi wa Kampuni ya simu ya Vodacom, Salum Mzee akizungumza wakati wa kukabidhi kpmpyuta tatu kwa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (CPC)

MKUU wa Wilaya ya Chamwino,Fatma Ally (kushoto) akimkabidhi kompyuta Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma Joyce Kasiki (kulia), katikati anayeshuhudia ni mwakilishi wa Kampuni ya simu ya Vodacom , Salum Mzee

Thursday, December 19, 2013

Watoto wasaidiwe kutohatarisha afya zao

Watoto Kijiji cha Mkakatika Wilaya ya bahi wakifurahia kuoga kwenye dimwi la maji ambayo si salama kufuatia mvua kuanza kunyesha kwenye wilaya hiyo
KUTOKANA na mvua kuanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dododoma, Wazazi wametakiwa kuwa makini na watoto wao ambao wengi wao wamekuwa wakipenda kuogolea katika madimbwi ya maji ikiwemo maji machafu.
 Kunyesha kwa mvua kumeleta shangwe kwa wakazi wengi wakiwemo watoto hali inayopelekea kuona hiyo ni fursa nzuri kwao kufurahia maji.
 Mkazi wa Bahi Mkoani Dodoma Pendo Alfonce alisema ni vizuri wazai wakawa makini kwa kuwazuia watoto wao kwenda kuoga kwani mvua zinazonyesha ni chache na maji yanayokjaa kwenye madimbwi pia ng'ombe wamekuwa wakitumia kunywa maji.
Watoto wa Kijiji cha Mkakatika Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wakioga kwente dimbwi la maji machafu.
 Alisema kumekuwa na tabia ya watoto kwenda kuoga kwenye madimbwi kitui ambacho ni hatari kwa afya zao kwani wana hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa mbalimbali ikiwemo kichocho.

Monday, December 16, 2013

Malkia wa Uholanzi azungumza na wakulima

Malkia wa Uholanzi azungumza na wakulima MALKIA wa Uholanzi Maxima ameshauri Seikali kuendelea na juhudi za wakulima na kuwatafutia masoko ya mazao wanayozalishwa. Alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi wa kilimo cha zabibu unayofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwenye Kijiji cha Gawae Manispaa ya Dodoma. Shamba hilo lina ekari 600, ekari 300 zimesafishwa na ekari 100 tayari limewekewa miundombinu ya uwagiliaji liko tayari kwa ajili ya kupandwa miche na kila mkulima atamiliki ekari moja . Malkia huyo alimwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na alikuwa ameongozana na Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayoshughulikia masuala ya kilimo na chakula Duniani ikiwemo WFP, Shirika la Chakula Duniani ( FAO) na Shirika la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Alisema wakulima wengi wanahitaji kusaidiwa ili waweze kuendesha kilimo chenye tija. Baadhi ya wakulima wa zabibu wakizungumza na malikia huyo walisema changamoto kubwa soko hali inayopelekea zabibu nyingi kuozea shambani. Lucy Mahelela alisema soko la zabibu haliji kwa wakati na hata linapokuja zabibu nyingine zinakuwa zimeshaanza kuoza. “Wanunuzi wengi hawanunui kwa wakati zabibu huanza kuozea shambani huku wengine wakitaka kuuziwa mchuzi wa zabibu” alisema Alisema hata wenye viwanda vidogovidogo wanataka kuuziwa mchuzi na si zabibu tena. “Hata zabibu zikiiva hawaji kununua na wanakuja kununua siku wanyotaka wao na kupanga bei wanayoitaka wao jambo ambalo linamuumiza mkulima kwani anauza kwa bei ya hasara ambayo hailingani na gharama za uzalishaji” alisema Pia kama soko lingekuwa na uhakika ana matumaini wakulima wengi wa zao hilo wangekuwa na mafanikio makubwa tofauti na sasa ambapo wamekuwa na soko la kubahatisha. Kwa upande wake John Ntandu alisema wamekuwa wakilima kwenye mashamba ambayo hayajapimwa hali inayowawia vigumu kupata mikopo kutoka kwenye mabenki hili kuendesha kwa ufanisi kilimo hicho. Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Robert Kitimbo alisema wamekusudia kukifanya kilimo cha zabibu kuwa na manufaa kwa wakulima na serikali imekuwa ikisaida katika miradi ya kilimo kama hiyo. Kwa upande wao wakulima kutoka Wilaya ya Chamwino ambao walipata msaada kutoka FAO, walisema wameongeza uzalishaji wa mazao na fedha walizopata kwa kuuza mazao hayo waliweza kununua zana bora za kilimo ikiwemo majembe ya kukokotwa na ng’ombe na hata pampu za umwagiliaji. Malkia Maxima wa Uholanzi akivishwa mavazi ya asili ya Wagogo, kaniki na kibuyu na mmoja wa wakulima wadogowadogo wa zabibu kijiji cha Gawae Manispaa ya Dodoma juzi alipofanya ziara kutembelea mradi huo unaofadhiliwa na WFP. Malkia Maxima wa Uholanzi akisisitiza jambo wakati alipokutana na Mkuu Wilaya ya Dodoma, Lephy Gembe (katikati) na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Robert Kitimbo (kushoto) wakati wakizungumzia namna ya kuendeleza mradi wa zabibu kijiji cha Gawae Manispaa ya Dodoma Malkia Maxima wa Uholanzi (kushoto) akimsalimia na mtoto Jenipher Andrew wakati alipofanya ziara kutembelea mradi wa kilimo cha zabibu unayofadhiliwa na WFP kwenye Kijiji cha Gawae Manispaa ya Dodoma mwishoni mwa wiki.

Thursday, December 12, 2013

Waimbaji kutoka Kenya, Somalia ndani ya tamasha la X mas

WAIMBAJI wa nyimbo za Injili kutoka ndani na nje ya Nchi wanatarajia kutubuiza katika Tamasha la kusifu la Shangwe za Xmas linalotarajia kufanyika desemba 25, mwaka huu Miongoni mwa wasanii kutoka nje ya nchi ni Tumsifu Rufutu kutoka Kenya . Msanii huyo anatamba na wimbo la Mwambie Farao, pi msanii mwingine ametajwa kuwa ni Mary Sinkala mwenye asili ya Somalia. Tamasha hilo litafanyika kwenye Uwanja wa jamhuri ambapo mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma wanatarajiwa kuhudhuria. Mary anatamba na wimbo wake wa wa Mkumbuke Muumba wako. Wasanii wengine watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo ni Beatrice William kutoka Jijini Dar es saalam aliyeanzia Bongo Star Search na kuamua kuokoka na kujikita kwenye nyimbo za injili huku akitamba na wimbo wa akina Delila wapo. Waimbaji wengine ni pamoja na Sospeter Jonas, Mzungu mzee wa Mshumaa Waimbaji hao wameshawataka wakazi wote wa mkoa wa Dodoma na vitongoji vyake kujitokeza kwa wingi kwani wamepanga kutoa burudani nzuri yenye lengo la kumtukuza na kumsifu Mungu na pia watawafundisha namna ya kumkumbuka muumba wao na jinsi ya kuelekea kaanani. Kiingilio katika tamasha hilo ni Sh 2,000 kwa wakubwa na Sh 1000 kwa watoto lengo likiwa ni kuwezesha watu wengi kumudu na kuhdhuria katika tamasha hilo. Tamasha hilo litawaunganisha waimbaji toka ndani ya nchi hasa wa mikoa ya DSM na Dodoma itakayobebwa na waimbaji toka makanisa mbalimbali na wachuo kikuu cha Dodoma (UDOM). Kwa mujibu wa mmoja wa waandaji wa tamasha hilo ambaye ni msemaji wa kampuni ya Liberty Promotion ,John Banda lengo la tamasha hilo ni pamoja na kuwachangia watoto yatima, wasiojiweza na wale walio katika mazingira magumu. Mwimbaji wa nyimbo za injili, Mary Sinkala ni miongoni mwa waimbaji watakaoshiriki Tamasha la Krismas litakalofanyika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, Desemba 25 mwaka huu.

Friday, December 6, 2013

Wajasiriamali wapatiwa mafunzo wa uwepo wa utengamano wa EAC

WAJASIRIAMALI Mkoani Dodoma wamepatiwa mafunzo ya kujengewa uelewa wa mchakato mzima wa uwepo wa mtengamano wa Jumuia ya Afrika Mashariki. Akifungua mafunzo hayo kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Mkoa wa Dodoma (TCCIA),Peter Ollomi alisema Tanzania ina wizara mahusus ya kusimamia na kuratibu uendelezaji wa mtangamano wa Jumuia ya Afrika Mashariki. Alisema dira ya wizara ni kuwa na Jumuia iliyoshamiri na inayowezesha Tanzania kunufaika kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuwa dhamira ya kuhakikisha Tanzania inashiriki kwa ufanisi katika kujenga jumuia ya Afrika mashariki iliyoshamiri na maslahi ya taifa yakizingatia vipaumbele vya Tanzania katika jumuia hiyo. Alivitaja vipengele hivyo kuwa ni kilimo na usalama wa chakula, viwanda, miundombinu kiuchumi, utalii na nishati. Aliwataka wajasiriamali kutumia fursa zilizopo katika mkoa ili kuweza kujiiunua kiuchumi. kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Mkoa wa Dodoma (TCCIA),Peter Ollomi akizungumza wakati wa mkutano huo. Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa wajasiriamali walengwa wa mtengamano wa Afrika Mashariki. Washiriki wa mafunzo kwa wajasiriamali walengwa wa mtengamano wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake akemea ukeketaji

DAKTARI bingwa wa magonjwa ya kinamama katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma Dk Januarius Hinju amesema kinamama wajawazito 4,130 kati ya 20,361 waliojifungua katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma katika kipindi cha mwaka 2011 na 2012 walikuwa wamekeketwa. Kauli hiyo ameitoa wakati wa mdahalo wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kanda ya kati. Dk.Hinju alisema kwa mwaka 2011 jumla ya akinamama wajawazito 10,477 waliojifungua katika hospitali ya mkoa ambapo katiyao 2392 sawa na asilimia 23 walikuwa wamekeketwa ikiwa ni sawa na asilimia 56. Amesema kutokana na kukeketwa walikuwa na tatizo la kutokwa na damu nyingi hali iliyosababisha kuhatarisha kupoteza maisha. Aidha mwaka 2012 jumla ya kinamama wajawazito 9914 walijifungua ambapo kati yao 1748 walikuwa wamekeketwa wakiwa sawa na asilimia 62. Dk Hinju amesema ipo haja ya ya kufanyika utafiti wa kina ili kubaini tatizo la ukeketaji katika mkoa wa Dodoma limepungua au la kutokana na vitendo vya ukeketaji kuhatarisha maisha ya wanawake wengi wakati wa kujifungua. Amesema takwimu hizo ni za waliojifungulia katika hospitali ya mkoa pekee hali inayoonesha kuna uwezekano kuwa tatizo la ukeketaji badili linaendelea katika jamii. Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma Januarius Hinju akizungumza wakati wa mdahalo wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kanda ya kati.Mdahalo huo uliandaliwa na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) unaoratibiwa na Shirika Lisilokuwa la Kiserikali la AFNET kwa kushirikiana na Shirika la WILFAF

Wednesday, December 4, 2013

Dhana ya maji ya Mungu yasichangiwe yakera wataalamu

WANANCHI waishio Vijijini Mkoani Dodoma wametakiwa kuona umuhimu wa kuchangia huduma za maji na kuondokana na dhana kuwa Maji ni ya Mungu yanatakiwa kutolewa bure. Mhandisi wa Maji Mkoa wa Dodoma Bazil Mwiserya alisema hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi . Alisema kuwa kuna baadhi ya maeneo Mkoani Dodoma ambayo miradi ya maji inatekelezwa wananchi wamekuwa wagumu kuchangia hali inayokwamisha miradi hiyo kuwa endelevu. “Jamii ihamasishwe kuchangia maji, unaweza kuona kuna mradi mkubwa wa maji lakini watu wanachota bure, jamii haitaki kuchangia imani yao maji ni ya Mungu yanatakiwa kutolewa bure” alisema. Mhandisi huyo alisema kwenye mtandao wa maji lazima watu wachangie ili fedha zitakazopatikana zitumike kwenye ukarabati. Alisema miradi mipya ya maji inayojengwa kuanzia sasa haitakabidhiwa kabla vyombo huru vya watumiaji kuundwa lengo likiwa ni kuwezesha wanachi kuchangia. “Hata kama ni kuchangia Sh. 50 kwa ndoo moja baada ya mwezi kutakuwa na fedha itakayopatikana ili kutumika kuendesha mradi wa maji” alisema Akielezea changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji katika Mkoa wa Dodoma alisema wataalam washauri wa makampuni binafsi hawatoi ushirikiano wa kutosha wakati wa utekelezaji wa miradi ya maji. Akitoa mfano alisema kuna mradi wa maji Mvumi Makulu Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, mkandarasi alisimama kuendelea na ujenzi wa mradi kwa kusubiri maelekezo ya mtaalam mshauri ili aweze kuendelea na kazi. Alisema masuala kama hayo yanakwamisha miradi kukamilika kwa wakati kwani mshauri anatakiwa kuwepo kutoa maelezo kipindichote cha kutekeleza mradi. Pia uwezo mdogo wa wakandarasi katika kutekeleza majukumu yao kifedha na hata watumishi bado ni tatizo. “”Sisi tunapotaka vigezo wanakuwa wamekamilisha vigezo hivyo lakini baada ya kazi kuanza ndipo unaona kusuasua kwa utekelezaji” alisema Alisema makandarasi wamekuwa wakiomba kazi zaidi ya moja na wakati mwingine kwa mikoa tofuati hali inayosababisha kuchelewa kukamilisha miradi kama ilivyo kwenye mikataba. Alisema Wilaya ya Kondoa na Chemba kuna miradi 13 ya maji, Bahi miradi saba, Manispaa Dodoma miradi 10, Chamwino miradi saba, Mpwapwa miradi sita na Kongwa Miradi tisa.

Waziri Kabaka aitaka NSSF kushirikiana na watoa huduma za fao la matibabu


WAZIRI  wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka amelitaka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)  ambalo linatoa fao la matibabu kushirikiana na watoa huduma kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora za matibabu.
Alitoa kauli hiyo leo Mjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa sita wa watoa huduma ya matibabu kwa mpango wa fao la matibabu.

Waziri Kabaka aliwakumbusha watoa huduma kushirikiana na NSSF katika kuboresha na kuimarisha mafao hayo kwa kutoa huduma nzuri na bora za matibabu kwa wanachama wa NSSF pamoja na wategemezi wao walioainishwa na kanuni za fao la matibabu.

Alisema wajibu mwingine kwa watoa huduma ni kuhakikisha wanawaelewesha wanachama wa SHIB kuhusu stahili zao na mipaka yao ya matibabu chini ya mpango wa SHIB bila kuwachanganya au kuwalipisha gharama mara mbili.

Kabaka alisema katika kipindi hiki fao la matibabu  limepitia changamoto mbalimbali ikiwemo viwango vya huduma zisizoridhisha  kwa baadhi ya watoa huduma, wanachama kutopewa huduma stahili wanapofika kwa watoa huduma kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa dawa.

Pia ufahamu mdogo wa wanachama juu ya stahili yao ya kupta matibabu bila malipo kutoka NSSF, baadhi ya wanachama kusita kujiandikisha kwa dhana kwamba watakatwa mafao yao wakati wnapofika umri wa kustaafu wakati si kweli pamoja na watoa huduma kutowasilisha NSSF takwimu sahihi  mafao ya matibabu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau alisema pamoja na mafanikio wanashuhudia baadhi ya watoa huduma yaani hospitali wanatoa huduma chini ya kiwango.

Alisema mpango huo wa fao la matibabu unafanyiwa maboresho ya kimfumo ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Dk.Dau alisema NSSF kwa kushirikiana na  na taasisi ya PharmAccess International imeanza utaratibu wa  kufanya tathimini kwa watoa huduma .
 
 

Mradi wa maji Ntomoko waanza kufufuliwa

ZAIDI ya wananchi 28,987 watanufaika mradi wa maji wa Ntomoko uliopo Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma ambapo shughuli za ujenzi na ukarabati unatarajia kuanza hivi karibuni. Hayo yamesemwa na Mhandisi wa Maji Mkoa wa Dodoma, Bazil Mwiserya wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi. Amesema mradi huo utanufaisha wananchi wa vijiji 10 wapatao 28,987. Mwanzoni mradi huo ulilenga vijiji 17 lakini vijiji 10 tu ndiyo vitaingia kwenye mradi wa ukarabati wa Ntomoko na vijiji vingine vitano vinatarajiwa kutafutiwa vyanzo vingine. Mhandisi huyo amesema kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa chujio la maji, ujenzi wa matanki mawili yenye ujazo wa lita 100,000 kila moja, ujenzi wa tanki moja lenye ujazo wa lita 90,000, ukarabati wa matanki a saba yenye ujazo wa lita 70,000 pamoja na ukarabati wa tanki moja lenye ujazo wa lita 50,000. Kazi nyingine ni ulazaji wa mabomba yenye vipenyo tofauti katika urefu wa jumla ya kilomita 94,926.Pia ujenzi wa vituo 61 vya kusambazia maji na ujenzi wa malambo 60 ya kunyweshea mifugo. Wataalamu waliamua kubadilisha teknolojia ya mabomba na kutumia mabomba ya plastiki badala ya chuma kwa kuwa yameathiriwa na kutu kutokana na aina ya udongo na hata chumvichumvi iliyo kwenye maji. Mradi huo uliojengwa miaka ya 1970 ulisimama kutokana na uchakavu wa miundombinu pamoja na uharibifu wa mazingira uliosababishwa zaidi na ukataji miti holela. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitembelea mradi huo mwaka jana na kuahidi Sh. bilioni mbili na andiko linaonekana kunahitajika Sh. Bilioni tatu. Mpaka sasa kiasi cha Sh. Bilioni moja zimeshapelekwa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kwa ajili ya utekelezaji ambapo kazi zilizofanyika mpaka sasa ni kukipatia maji kitongoji cha Fai kilicho karibu na chanzo cha maji ili kuwezesha wananchi wasifike kwenye chanzo ikiwa ni njia ya kutunza chanzo hicho. Ujenzi wa mradi huo mdogo ulitokana na agizo la Waziri ili wananchi wapate maji wakiwa kijijini bila kufika kwenye chanzo cha maji ikiwa ni njia ya utunzaji wa chanzo ili wananchi waone chanzo ni chao na kinawasaidia na wanajukumu la kuhakikisha kinaunzwa. imeelezwa tathimini ya kumpata kandarasi kwa ajili ya kuanza kujenga miundombinu katika vijiji imefanyika na utekelezaji unatarajia kuanza mwezi huu.Mradi huo unatakiwa kukamilika ndani ya miezi sita. Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maji, Dk.Binilith Mahenge alitembelea mradi huo wa Ntomoko na kuagiza watendaji kuhakikisha mradi huo na miradi mingine inatekelezwa ili kuondoa kero ya upatikanaji wa maji.