Wednesday, December 4, 2013

Dhana ya maji ya Mungu yasichangiwe yakera wataalamu

WANANCHI waishio Vijijini Mkoani Dodoma wametakiwa kuona umuhimu wa kuchangia huduma za maji na kuondokana na dhana kuwa Maji ni ya Mungu yanatakiwa kutolewa bure. Mhandisi wa Maji Mkoa wa Dodoma Bazil Mwiserya alisema hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi . Alisema kuwa kuna baadhi ya maeneo Mkoani Dodoma ambayo miradi ya maji inatekelezwa wananchi wamekuwa wagumu kuchangia hali inayokwamisha miradi hiyo kuwa endelevu. “Jamii ihamasishwe kuchangia maji, unaweza kuona kuna mradi mkubwa wa maji lakini watu wanachota bure, jamii haitaki kuchangia imani yao maji ni ya Mungu yanatakiwa kutolewa bure” alisema. Mhandisi huyo alisema kwenye mtandao wa maji lazima watu wachangie ili fedha zitakazopatikana zitumike kwenye ukarabati. Alisema miradi mipya ya maji inayojengwa kuanzia sasa haitakabidhiwa kabla vyombo huru vya watumiaji kuundwa lengo likiwa ni kuwezesha wanachi kuchangia. “Hata kama ni kuchangia Sh. 50 kwa ndoo moja baada ya mwezi kutakuwa na fedha itakayopatikana ili kutumika kuendesha mradi wa maji” alisema Akielezea changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji katika Mkoa wa Dodoma alisema wataalam washauri wa makampuni binafsi hawatoi ushirikiano wa kutosha wakati wa utekelezaji wa miradi ya maji. Akitoa mfano alisema kuna mradi wa maji Mvumi Makulu Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, mkandarasi alisimama kuendelea na ujenzi wa mradi kwa kusubiri maelekezo ya mtaalam mshauri ili aweze kuendelea na kazi. Alisema masuala kama hayo yanakwamisha miradi kukamilika kwa wakati kwani mshauri anatakiwa kuwepo kutoa maelezo kipindichote cha kutekeleza mradi. Pia uwezo mdogo wa wakandarasi katika kutekeleza majukumu yao kifedha na hata watumishi bado ni tatizo. “”Sisi tunapotaka vigezo wanakuwa wamekamilisha vigezo hivyo lakini baada ya kazi kuanza ndipo unaona kusuasua kwa utekelezaji” alisema Alisema makandarasi wamekuwa wakiomba kazi zaidi ya moja na wakati mwingine kwa mikoa tofuati hali inayosababisha kuchelewa kukamilisha miradi kama ilivyo kwenye mikataba. Alisema Wilaya ya Kondoa na Chemba kuna miradi 13 ya maji, Bahi miradi saba, Manispaa Dodoma miradi 10, Chamwino miradi saba, Mpwapwa miradi sita na Kongwa Miradi tisa.

No comments:

Post a Comment