Malkia wa Uholanzi azungumza na wakulima
MALKIA wa Uholanzi Maxima ameshauri Seikali kuendelea na juhudi za wakulima na kuwatafutia masoko ya mazao wanayozalishwa.
Alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi wa kilimo cha zabibu unayofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwenye Kijiji cha Gawae Manispaa ya Dodoma.
Shamba hilo lina ekari 600, ekari 300 zimesafishwa na ekari 100 tayari limewekewa miundombinu ya uwagiliaji liko tayari kwa ajili ya kupandwa miche na kila mkulima atamiliki ekari moja .
Malkia huyo alimwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na alikuwa ameongozana na Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayoshughulikia masuala ya kilimo na chakula Duniani ikiwemo WFP, Shirika la Chakula Duniani ( FAO) na Shirika la Maendeleo ya Kilimo (IFAD)
Alisema wakulima wengi wanahitaji kusaidiwa ili waweze kuendesha kilimo chenye tija.
Baadhi ya wakulima wa zabibu wakizungumza na malikia huyo walisema changamoto kubwa soko hali inayopelekea zabibu nyingi kuozea shambani.
Lucy Mahelela alisema soko la zabibu haliji kwa wakati na hata linapokuja zabibu nyingine zinakuwa zimeshaanza kuoza.
“Wanunuzi wengi hawanunui kwa wakati zabibu huanza kuozea shambani huku wengine wakitaka kuuziwa mchuzi wa zabibu” alisema
Alisema hata wenye viwanda vidogovidogo wanataka kuuziwa mchuzi na si zabibu tena.
“Hata zabibu zikiiva hawaji kununua na wanakuja kununua siku wanyotaka wao na kupanga bei wanayoitaka wao jambo ambalo linamuumiza mkulima kwani anauza kwa bei ya hasara ambayo hailingani na gharama za uzalishaji” alisema
Pia kama soko lingekuwa na uhakika ana matumaini wakulima wengi wa zao hilo wangekuwa na mafanikio makubwa tofauti na sasa ambapo wamekuwa na soko la kubahatisha.
Kwa upande wake John Ntandu alisema wamekuwa wakilima kwenye mashamba ambayo hayajapimwa hali inayowawia vigumu kupata mikopo kutoka kwenye mabenki hili kuendesha kwa ufanisi kilimo hicho.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Robert Kitimbo alisema wamekusudia kukifanya kilimo cha zabibu kuwa na manufaa kwa wakulima na serikali imekuwa ikisaida katika miradi ya kilimo kama hiyo.
Kwa upande wao wakulima kutoka Wilaya ya Chamwino ambao walipata msaada kutoka FAO, walisema wameongeza uzalishaji wa mazao na fedha walizopata kwa kuuza mazao hayo waliweza kununua zana bora za kilimo ikiwemo majembe ya kukokotwa na ng’ombe na hata pampu za umwagiliaji.

Malkia Maxima wa Uholanzi akivishwa mavazi ya asili ya Wagogo, kaniki na kibuyu na mmoja wa wakulima wadogowadogo wa zabibu kijiji cha Gawae Manispaa ya Dodoma juzi alipofanya ziara kutembelea mradi huo unaofadhiliwa na WFP.

Malkia Maxima wa Uholanzi akisisitiza jambo wakati alipokutana na Mkuu Wilaya ya Dodoma, Lephy Gembe (katikati) na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Robert Kitimbo (kushoto) wakati wakizungumzia namna ya kuendeleza mradi wa zabibu kijiji cha Gawae Manispaa ya Dodoma

Malkia Maxima wa Uholanzi (kushoto) akimsalimia na mtoto Jenipher Andrew wakati alipofanya ziara kutembelea mradi wa kilimo cha zabibu unayofadhiliwa na WFP kwenye Kijiji cha Gawae Manispaa ya Dodoma mwishoni mwa wiki.
No comments:
Post a Comment