Wednesday, December 4, 2013

Mradi wa maji Ntomoko waanza kufufuliwa

ZAIDI ya wananchi 28,987 watanufaika mradi wa maji wa Ntomoko uliopo Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma ambapo shughuli za ujenzi na ukarabati unatarajia kuanza hivi karibuni. Hayo yamesemwa na Mhandisi wa Maji Mkoa wa Dodoma, Bazil Mwiserya wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi. Amesema mradi huo utanufaisha wananchi wa vijiji 10 wapatao 28,987. Mwanzoni mradi huo ulilenga vijiji 17 lakini vijiji 10 tu ndiyo vitaingia kwenye mradi wa ukarabati wa Ntomoko na vijiji vingine vitano vinatarajiwa kutafutiwa vyanzo vingine. Mhandisi huyo amesema kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa chujio la maji, ujenzi wa matanki mawili yenye ujazo wa lita 100,000 kila moja, ujenzi wa tanki moja lenye ujazo wa lita 90,000, ukarabati wa matanki a saba yenye ujazo wa lita 70,000 pamoja na ukarabati wa tanki moja lenye ujazo wa lita 50,000. Kazi nyingine ni ulazaji wa mabomba yenye vipenyo tofauti katika urefu wa jumla ya kilomita 94,926.Pia ujenzi wa vituo 61 vya kusambazia maji na ujenzi wa malambo 60 ya kunyweshea mifugo. Wataalamu waliamua kubadilisha teknolojia ya mabomba na kutumia mabomba ya plastiki badala ya chuma kwa kuwa yameathiriwa na kutu kutokana na aina ya udongo na hata chumvichumvi iliyo kwenye maji. Mradi huo uliojengwa miaka ya 1970 ulisimama kutokana na uchakavu wa miundombinu pamoja na uharibifu wa mazingira uliosababishwa zaidi na ukataji miti holela. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitembelea mradi huo mwaka jana na kuahidi Sh. bilioni mbili na andiko linaonekana kunahitajika Sh. Bilioni tatu. Mpaka sasa kiasi cha Sh. Bilioni moja zimeshapelekwa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kwa ajili ya utekelezaji ambapo kazi zilizofanyika mpaka sasa ni kukipatia maji kitongoji cha Fai kilicho karibu na chanzo cha maji ili kuwezesha wananchi wasifike kwenye chanzo ikiwa ni njia ya kutunza chanzo hicho. Ujenzi wa mradi huo mdogo ulitokana na agizo la Waziri ili wananchi wapate maji wakiwa kijijini bila kufika kwenye chanzo cha maji ikiwa ni njia ya utunzaji wa chanzo ili wananchi waone chanzo ni chao na kinawasaidia na wanajukumu la kuhakikisha kinaunzwa. imeelezwa tathimini ya kumpata kandarasi kwa ajili ya kuanza kujenga miundombinu katika vijiji imefanyika na utekelezaji unatarajia kuanza mwezi huu.Mradi huo unatakiwa kukamilika ndani ya miezi sita. Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maji, Dk.Binilith Mahenge alitembelea mradi huo wa Ntomoko na kuagiza watendaji kuhakikisha mradi huo na miradi mingine inatekelezwa ili kuondoa kero ya upatikanaji wa maji.

No comments:

Post a Comment