Thursday, November 28, 2013

Waziri Kabaka ataka kuboreshwa kwa fao la matibabu


WAZIRI  wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka amelitaka Shirika la taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)  ambalo linatoa fao la matibabu kushirikiana na watoa huduma kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora za matibabu.
Alitoa kauli hiyo leo Mjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa sita wa watoa huduma ya matibabu kwa mpango wa fao la matibabu.

Waziri Kabaka aliwakumbusha watoa huduma kushirikiana na NSSF katika kuboresha na kuimarisha mafao hayo kwa kutoa huduma nzuri na bora za matibabu kwa wanachama wa NSSF pamoja na wategemezi wao walioainishwa na kanuni za fao la matibabu.

Aidha alisema wajibu mwingine kwa watoa huduma ni kuhakikisha wanawaelewesha wanachama wa SHIB kuhusu stahili zao na mipaka yao ya matibabu chini ya mpango wa SHIB bila kuwachanganya au kuwalipisha gharama mara mbili.

Kabaka alisema katika kipindi hiki fao la matibabu  limepitia changamoto mbalimbali ikiwemo viwango vya huduma zisizoridhisha  kwa baadhi ya watoa huduma, wanachama kutopewa huduma stahili wanapofika kwa watoa huduma kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa dawa.

Pia ufahamu mdogo wa wanachama juu ya stahili yao ya kupta matibabu bila malipo kutoka NSSF, baadhi ya wanachama kusita kujiandikisha kwa dhana kwamba watakatwa mafao yao wakati wnapofika umri wa kustaafu wakati si kweli pamoja na watoa huduma kutowasilisha NSSF takwimu sahihi  mafao ya matibabu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau alisema pamoja na mafanikio wanashuhudia baadhi ya watoa huduma yaani hospitali wanatoa huduma chini ya kiwango.

Kulingana na kauli yake, mpango huo wa fao la matibabu unafanyiwa maboresho ya kimfumo ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Dk.Dau alisema NSSF kwa kushirikiana na  na taasisi ya PharmAccess International imeanza utaratibu wa  kufanya tathimini kwa watoa huduma .

No comments:

Post a Comment