Thursday, November 28, 2013

Waziri Kabaka ataka kuboreshwa kwa fao la matibabu


WAZIRI  wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka amelitaka Shirika la taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)  ambalo linatoa fao la matibabu kushirikiana na watoa huduma kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora za matibabu.
Alitoa kauli hiyo leo Mjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa sita wa watoa huduma ya matibabu kwa mpango wa fao la matibabu.

Waziri Kabaka aliwakumbusha watoa huduma kushirikiana na NSSF katika kuboresha na kuimarisha mafao hayo kwa kutoa huduma nzuri na bora za matibabu kwa wanachama wa NSSF pamoja na wategemezi wao walioainishwa na kanuni za fao la matibabu.

Aidha alisema wajibu mwingine kwa watoa huduma ni kuhakikisha wanawaelewesha wanachama wa SHIB kuhusu stahili zao na mipaka yao ya matibabu chini ya mpango wa SHIB bila kuwachanganya au kuwalipisha gharama mara mbili.

Kabaka alisema katika kipindi hiki fao la matibabu  limepitia changamoto mbalimbali ikiwemo viwango vya huduma zisizoridhisha  kwa baadhi ya watoa huduma, wanachama kutopewa huduma stahili wanapofika kwa watoa huduma kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa dawa.

Pia ufahamu mdogo wa wanachama juu ya stahili yao ya kupta matibabu bila malipo kutoka NSSF, baadhi ya wanachama kusita kujiandikisha kwa dhana kwamba watakatwa mafao yao wakati wnapofika umri wa kustaafu wakati si kweli pamoja na watoa huduma kutowasilisha NSSF takwimu sahihi  mafao ya matibabu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau alisema pamoja na mafanikio wanashuhudia baadhi ya watoa huduma yaani hospitali wanatoa huduma chini ya kiwango.

Kulingana na kauli yake, mpango huo wa fao la matibabu unafanyiwa maboresho ya kimfumo ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Dk.Dau alisema NSSF kwa kushirikiana na  na taasisi ya PharmAccess International imeanza utaratibu wa  kufanya tathimini kwa watoa huduma .

Wednesday, November 27, 2013

Mfugaji asema wanajiua wenyewe hawalogwi

Nduluyaluha Wile Lusendamila akiwa katika pozi.

 .Yeye amebadilika anaenda kisasa
MFUGAJI kutoka Kijiji cha Uhelela Wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma Nduluyaluha Wile Lusendamila amesema elimu ndogo waliyonayo wafugaji wengi inapelekea kuishi maisha ya kimaskini licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa mifugo.
Mfugajji huyo ni kati ya wafugaji walioamua kubadilika na kuvuna mifugo yao kwa ajili ya kustawisha maisha yao.
Alianza kuvuna mifugo yake mwaka 2008  ili aweze kuishi vizuri kutokana na kuwa na mifugo mingi ambayo alikuwa haufurahii utajiri huo.
Mwaka 2004 wakati wa vuguvugu la kuhamisha wafugaji kutoka Ihefu Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya safari yake iliishia Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma ambapo aliamua kuweka maskani yake.Wakati akitoka Ihefu kwenda Bahi alikuwa na ng’ombe 1,700  na mbuzi zaidi ya 300 lakini mpaka sasa amebaki na ng’ombe 300 na maisha yake yamebadilika.
‘’Tumezaliwa kwenye mifugo hatuna elimu, naomba  wafugaji wabadilike watoto wao hawasomi sababu ya utumwa wa mifugo, tuifuge sio itufuge utajiri huu unaweza kubadilishwa na kumfanya mfugaji aongeze muda wa kuishi duniani” alisema
Lusendamila (kushoto aliyesimama) akiwa na  familia yake (Wa pili kushoto) mwenye kilemba ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi.

Kulingana na kauli yake, wafugaji wengi wamekuwa wakilala nyumba moja na mifugo jambo ambalo husababisha kuugua magonjwa mbalimbali ikiwemo kifua na hivyo kuwafanya kuwa dhaifu.
‘’Vumbi la ndani ya nyumba la kulala na mifugo ni hatari  hatulogwi tunajiua wenyewe” alisema
Sasa ameweza kujenga nyumba tatu za kisasa, kusomesha watoto kwenye shule za mchepuo wa Kiingereza, kununua magari ya kutembelea na amekuwa akimiliki daladala kwa ajili ya biashara.Pia kuwasaidia ndugu zake na wazazi wake.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Alfred Msovella akimzungumzia mfugaji huyo anasema ni mfano wa kuigwa kwani ameamua kuacha kuitumikia mifugo na sasa mifugo inamtumikia yeye.
Alisema ni vizuri elimu hiyo ikatolewa kwa wafugaji katika maeneo mengine nchini ambapo ina nafasi kubwa katika uunzaji wa mazingira na kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
‘’Alipokuwa Ihefu alionekana kama adui hafai  kumbe kinachotakiwa kufanyika ni kuelimisha wafugaji” alisema
 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk.Rehema Nchimbi akipanda mti  nyumbani kwa mfugaji huyo Kijiji cha Uhelela Wilaya ya Bahi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi anasema kuna haja ya kwapokea wafugaji na kuwaelimisha kisha watulie kwani ufugaji ni moja ya malengo muhimu katika uchumi na maendeleo katika Nchi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Bahi Betty Mkwasa jitihada zinaendelea za  kuhamasisha wafugaji  kuwa na mifugo inayoendana na uwezo wa malisho na itakayoboresha  maisha  ya wananchi na wafugaji.
 Anasema mipango hiyo ni ya muda mfupi, kati na mrefu wa uvunaji wa mifugo.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa akipanda mti nyumbani kwa mfugaji huyo

Mkwasa anasema mpaka sasa wafugaji 68 wamevuna mifugo yao pia kuna mpango wa kuanzisha ushirika wa wafugaji utakao simamiwa na Benki yaCRDB.