Sunday, November 17, 2013

Chemba waanza mikakati kuunda vikundi vya vijana


MKUU wa Wilaya Mpya ya Chemba Mkoani Dodoma, Francis Isaack amesema tayari Wilaya hiyo imeanza mikakati ya kuunda vikundi vya vijana kwa lengo la kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo.

 Alisema hayo hivi karibuni katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi ambapo tayari amewaagiza watendaji wote wa Vijiji na Kata katika wilaya hiyo, kutokodisha mashamba ya vijiji na badala yake mashamba hayo wapatiwe vijana kwa ajili ya uzalishaji ili kuweza kuondokana na umaskini.

 “Tayari tumeanza mkakati wa kuunda vikundi vya Vijana katika vijiji vyote vya wilaya  ya Chemba,hivyo mashamba yote ya Serikali za Vijiji watapatiwa Vijana ambao wataendesha kilimo cha kisasa na chenye tija” Alisema  vijana hao watakuwa shamba darasa kwa familia zao na jamii inayowazunguka ambapo  pia mara baada ya Vijana hao kuvuna mazao yao ,watajikita katika shughuli za ufugaji wa nyuki .

Pia Mkuu huyo wa Wilaya alisema ujenzi wa nyumba na ofisi ya Mkuu wa Wilaya  hiyo inatarajia kukamilika Julai mwakani.
Alisema sasa wakandarasi wa ujenzi huo wanaendelea na hatua mbalimbali  za ujenzi na kuanzia Julai mwakani shughuli nyingi za kiserikali zitahamishiwa  Wilayani humo.
Aidha alibainisha kuwa Hospitali ya Wilaya ya Wilaya hiyo itajengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Serikali ambapo wananchi watachangia tofali,kokoto na mchanga.
Chemba ni Wilaya mpya katika Mkoa wa Dodoma iliyoanzishwa mwaka 2012  baada ya kugawanywa kwa  Wilaya ya Kondoa.

No comments:

Post a Comment