MKUU wa Wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma, Betty Mkwasa amewashutumu
baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa kuhujumu hifadhi ya msitu
wa Serikali wa Goima.
Mkwasa alitoa shutuma hizo hivi karibuni kwenye kikao cha Baraza la Madiwani
wakati wakijadili taarifa za utekelezaji wa miradi kwa mwaka 2013/14.
Kata hizo tatu zinazodaiwa kuhujumu hifadhi hiyo ya msitu ni
Msisi,Lamaiti na Ilindi ambazo ndani yake zimezungukwa na vijiji
vitano.
Alisema madiwani hao kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji
hivyo wamesababisha kuangamizwa kwa msitu huo kutokana na kupokea
rushwa ya fedha kutoka kwa wananchi ili waweze kukata miti na kulima
kwenye hifadhi hiyo.
Mkwasa alisema wamefikia hatua ya kuchaguana kwenye uongozi wa kamati
iliyoundwa kwenye kata hiyo ambapo mwenyekiti wake akiwa Diwani wa
Kata ya Msisi, Chuga Mgalilwa.
Pia alisema kamati hiyo kwa pamoja imekuwa ikipokea fedha kutoka kwa
watu mbalimbali wanaohitaji kulima na kukata miti,kuingiza mifugo bila
kujali kuwa viongozi hao wanatakiwa kuongoza katika kuulinda msitu huo
wa serikali.
Pia Mkwasa alisema mabango kwa ajili ya kuzuia kufanyika kwa shughuli
za kibinadamu yamekuwa yaking’olewa huku Diwani huyo akiwa hachukui
hatua zozote hali inayodhihirisha wazi wamedhamiria kuhujumu msitu huo
ambapo baadhi ya watu wameanza kuweka makazi yasiyo rasmi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Msisi, Chuga Mgalilwa akijibu
tuhuma hizo alisema kuwa madai ya Mkuu wa wilaya hayana ukweli wowote
bali yana nia ya kutaka kuchonganishwa na madiwani wezake na wananchi.
Mgalilwa alisema uvamizi unaofanyika katika msitu huo ni kutokana na
Serikali kuuacha kwa kipindi kirefu na wananchi wakaamua kuvamia kwa
shughuli za kilimo na ukataji wa miti.
Alisema sehemu kubwa ya msitu huo uko kwenye kata anayoiongoza na
hawezi kuzuia wapiga kura wake na wakamuelewa.
“Kwa upande wangu siwezi kuwazuia wapigakura wangu hao na
wakanielewa, siko tayari kukosa kura ”alisema.
Aidha alisema sehemu kubwa ya mazao inalimwa katika msitu huo ikiwemo
mahindi, ufuta alizeti na mpunga.
Alisema kabla ya uvamizi waliomba serikali kuwapa walinzi wea msitu
lakini serikali ilikaa kimya hali iliyosababisha wananchi kuvamia.
Hata hivyo, Afisa Ardhi Maliasili wa Wilaya ya Bahi, Godfrey Jeremiah
alisema hifadhi hiyo ya msitu ni ya Serikali yenye ukubwa wa ekari
6957 ikiwa na uoto wa asili.
Alisema tatizo lililopo ni kwa watendaji wa vijiji ambavyo
vinavyozunguka hifadhi hiyo wanaruhusu wananchi kuutumia kwa kilimo na
ukataji wa miti hali inayopelekea uharibifu mkubwa ndani ya hifadhi
hiyo.
No comments:
Post a Comment