Wednesday, November 6, 2013

Chiboli hali tete

BAADHI ya wakazi wa Kijiji cha Chiboli, wilaya ya Chamwino Mkoani hapa hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa.
Akizungumza  Kijijini hapo, Diwani wa Kata ya Chiboli, William Teyu alisema mvua hiyo ilinyesha juzi kuanzia saa 11 jioni  na kudumu zaidi ya saa moja.
Alisema madhara yaliyosababishwa na mvua hiyo ni pamoja na kuezuliwa kwa nyumba 11 na uharibifu wa vitu mbalimbali vikiwemo vyakula, umeme wa jua ,radio na simu.
Diwani huyo alisema miongoni mwa nyumba zilizoezuliwa nane kati ya nyumba hizo  ni za wananchi wa kawaida,mbili nyumba za walimu na moja ya kwake mwenyewe (Diwani)
Alisema kutokana na janga hilo wananchi hao hivi sasa wanaishi kwa majrani huku wengine wakiishi kwenye vyumba walivyokuwa wakivitumia kama majiko ya kupikia na stoo za kuhifadhia chakula.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Adrian Jungu ameahidi kupeleka wataalamu kwa ajili ya kufanya tathimini kuhusu madhara yaliyosababisha na mvua hiyo.
Pamoja na hayo alisema wataangalia namna ya kuwasaidia wananchi waliopata madhara hayo.

No comments:

Post a Comment